• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
NMG kutumia majukwaa yake kupeperusha mbio za London Marathon moja kwa moja

NMG kutumia majukwaa yake kupeperusha mbio za London Marathon moja kwa moja

Na CHRIS ADUNGO

KAMPUNI ya Nation Media Group (NMG) itapeperusha moja kwa moja makala ya 40 ya mbio za London Marathon mnamo Oktoba 4, 2020, kupitia runinga za NTV Kenya na Uganda.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NMG, Stephen Gitagama amesema itakuwa fahari sana kwa kampuni hiyo kupeperusha kivumbi hicho kupitia runinga zao pamoja na mtandao wa Natio.Africa.

“Tunawakaribisha Wakenya wote kumtazama bingwa wa dunia na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon, Eliud Kipchoge akiwaongoza Wakenya wenzake kutifuana na Kenenisa Bekele jijini London. Tunawatakia wanariadha wa Kenya kila la heri,” akasema Gitagama wakati wa kuzinduliwa kwa mpango huo wa NMG mnamo Septemba 9, 2020.

Mkuu wa Kitengo cha Matangazo katika NMG, Monica Ndung’u, alisema hatua ya NMG kupata haki za kupeperusha London Marathon moja kwa moja ni ya kimakusudi hasa ikizingatiwa umaarufu wa mchezo wa riadha miongoni mwa Wakenya.

“Inaridhisha sana hasa ikizingatiwa kwamba hili ni jambo linalofanyika wakati ambapo matukio mengi katika ulingo wa riadha hajafanyika kwa sababu ya janga la corona. Ni fahari tele kwamba NTV itawapa Wakenya fursa ya kufuatilia mbio za London Marathon moja kwa moja na kuwatilia shime wanariadha wao,” akasema Ndung’u kwa kuwataka Wakenya kuwa sehemu ya historia ya mbio hizo kupitia #LetsgoKenya.

Mbali na Kipchoge, Wakenya wengine watakaonogesha kivumbi cha London Marathon kwa upande wa wanawake ni Ruth Chepng’etich, Vivian Cheruiyot na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon, Brigid Kosgei.

“Nina hakika Wakenya watatamba katika mbio hizo na kupeperusha vyema bendera ya taifa letu,” akasema Ndung’u kwa kushikilia kwamba Waganda wamekuwa tishio kubwa kwa Wakenya katika miaka ya hivi karibuni ambayo imewashuhudia wakiinukia vyema katika mbio za masafa marefu.

Mhariri wa Spoti katika NMG, Elias Makori alisema ni fahari tele kwa NMG kupata haki za kupeperusha mbio za London Marathon moja kwa moja hasa baada ya marathon kuu nyinginezo duniani za Boston, Chicago, Berlin na New York City kufutiliwa mbali mwaka huu kwa sababu ya corona.

“Kufaulu kwa NTV kupata idhini ya kupeperusha mbio hizo ni ithibati kwamba ndiyo runinga inayoaminiwa zaidi na Wakenya kwa sababu ya ubora wa matangazo yake ya habari na upeperushaji wa vipindi,” akasema Makori katika kauli iliyotiliwa mkazo na Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Masuala ya Nje katika NMG, Clifford Machoka.

  • Tags

You can share this post!

Wafahamu mbwa bora katika shughuli za ulinzi

CoG yashutumiwa kwa kuzima matangazo ya biashara na NMG