• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Ralf Rangnick apokezwa mikoba ya timu ya taifa ya Austria

Ralf Rangnick apokezwa mikoba ya timu ya taifa ya Austria

Na MASHIRIKA

KOCHA mshikilizi wa Manchester United, Ralf Rangnick, 63, ameteuliwa kuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya Austria.

Ametia saini mkataba wa miaka miwili na ataanza kutekeleza majukumu yake mnamo Mei 2022 baada ya kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kukamilika.

Rangnick ambaye ni raia wa Ujerumani, bado atasalia kuwa mshauri wa benchi ya kiufundi ya Man-United jinsi ilivyopangwa na kikosi hicho kabla ya kuteuliwa kwa mkufunzi Erik ten Hag wa Ajax atakayetua ugani Old Trafford mwishoni mwa msimu huu.

“Ningali na ndoto ya kusaidia Man-United kufikia mahali inakostahili ili irejeshe uthabiti wake wa zamani. Hilo ndilo jambo ninalotazamia,” akasema Rangnick.

“Ni tija na fahari tele kupokezwa mikoba ya Austria ambayo natazamia kuongoza katika fainali zijazo za Euro nchini Ujerumani,” akaongeza.

Austria ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 23 kwenye orodha ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), wamekuwa bila kocha tangu Franco Foda ajiuzulu mnamo Machi 2022 baada ya kikosi hicho kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar kati ya Novemba na Disemba 2022.

Man-United wameshinda mechi 10 kati ya 25 za mashindano yote msimu huu chini ya Rangnick aliyejaza nafasi ya Ole Gunnar Solskjaer aliyetimuliwa ugani Old Trafford mnamo Novemba 2021.

Kufikia sasa, mabingwa hao mara 20 wa EPL wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la kipute hicho huku pengo la alama tano zikitamalaki kati yao na Arsenal wanaofunga orodha ya nne-bora. Zimesalia mechi tatu pekee kabla ya kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi.

Ten Hag ndiye kocha wa tano kuajiriwa na Man-United kwa mkataba wa kudumu tangu 2013 baada ya mkufunzi Sir Alex Ferguson kustaafu.

Rangnick alikuwa mkuu wa maendeleo ya soka kambini mwa Lokomotiv Moscow nchini Urusi kabla ya kutua Man-United. Amewahi pia kudhibiti mikoba ya klabu za Ulm, Stuttgart, Hannover, Hoffenheim, Schalke na RB Leipzig. Aliwahi kutwaa taji la German Cup na kuongoza Schalke 04 kutinga nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2011.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Man-United na Chelsea nguvu sawa katika gozi la EPL ugani...

Jinsi Kibaki alivyokaidi Kenyatta mara 2

T L