• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 12:45 AM
Rubis yawaweka sawa madereva Safari Rally ikianza

Rubis yawaweka sawa madereva Safari Rally ikianza

Na GEOFFREY ANENE

DEREVA Jasmeet Chana amesema ni afueni kubwa kuondolewa mzigo wa kujigharimia kila kitu kwenye mashindano ya mbio za magari.

Hiyo ni baada ya kampuni ya kuuza mafuta ya Rubis Energy Kenya kumpiga jeki jana Jumatano kabla ya Safari Rally 2023.

Jasmeet anayeshirikiana na ndugu yake Ravinder Chana katika gari la Mitsubishi Lancer Evo X anaongoza Mbio za Magari za Kitaifa Kenya (KNRC) baada ya kuandikisha nambari tatu Machakos Rally na Equator Rally na kushinda Nakuru Rally.

“Udhamini huu wa Rubis ni wangu wa kwanza kabisa kutoka kwa shirika. Naufurahia sana. Unanipa motisha kubwa ya kupaisha gari kwa asilimia 100 ili kupata matokeo mazuri,” alisema Jasmeet.

Alifichua kuwa lengo lao ni kumaliza kitengo cha KNRC katika nafasi ya kwanza wakati wa duru hiyo ya saba ya Mbio za Magari Duniani (WRC) jijini Nairobi na eneo la Naivasha katika kaunti ya Nakuru.

Jasmeet atakuwa akishiriki Safari Rally kwa mara yake ya 17 tangu aanze mashindano ya magari 2007.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Rubis Energy East Africa na Mkurugenzi Mkuu wa Rubis Energy Kenya Jean-Christian Bergeron alisema kuwa kupitia udhamini huo, Jasmeet, 45, aliyekamata nafasi ya 14 kati ya washiriki 42 kwenye Safari Rally 2022, atapata mafuta na bidhaa nyingine za Castro atahitaji.

Dereva Issa Amwari atakaelekezwa na Dennis Mwenda katika Mitsubishi Lancer Evo X pia alinufaika na udhamini sawa na huo kutoka Rubis Energy Kenya.

Aidha, dereva Thierry Neuville ametangaza kushirikiana na shirika la mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za marathon Eliud Kipchoge la mazingira na elimu wakati huu wa Safari Rally.

“Kupitia shirika lake, Eliud anawapa watoto zaidi fursa ya kupata elimu kwa kuwalipia karo na pia kujenga maktaba. Shirika lake pia linashughulikia kulinda mazingira kwa kupanda miti katika misitu iliyoharibiwa na pia upanzi wa miti ya matunda na mboga kote nchini,” akasema dereva huyo Mbelgiji kwenye mtandao wake wa kijamii.

Neuville aliongeza kuwa Eliud analinda mazingira ili kizazi kijacho kipate kufaidika na mazingira mazuri.

“Majuzi alitwaa ekari 130 za msitu wa Kaptagat karibu na kambi yake ya mazoezi na ninafurahi kusaidia miradi hii muhimu,” alisema Neuville, 35.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume akiri kuiba jozi ya viatu msikitini

Mwanamume ashtakiwa kwa kulaghai muuzaji wa dawa ya sumu ya...

T L