• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Steven Gerrard achukua mikoba ya Al-Ettifaq

Steven Gerrard achukua mikoba ya Al-Ettifaq

Na MASHIRIKA

ALIYEKUWA kiungo wa Liverpool na timu ya taifa ya Uingereza, Steven Gerrard, ameteuliwa kuwa kocha wa kikosi cha Al-Ettifaq nchini Saudi Arabia.

Mnamo Juni 2023, sogora huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 43 alisema alikuwa amealikwa nchini Saudi Arabia “kutafuta ofa kadhaa za ukocha” ila akasisitiza kuwa asingekubali kazi ya ukufunzi katika taifa hilo.

“Bila shaka, kuwepo kwa Gerrard, ambaye anajivunia maarifa tele katika soka, kutaongeza thamani kubwa katika ligi yetu,” akasema mwenyekiti wa Al-Ettifaq, Khalid Al-Dabal.

Gerrard ametia saini mkataba wa miaka miwili kambini mwa kikosi hicho cha Saudia.

Al-Ettifaq walikuwa wa saba katika orodha ya vikosi 16 katika kipute cha Saudi Pro League msimu wa 2022-23 na walikamilisha kampeni kwa alama 35 nyuma ya Al-Ittihad waliotawazwa mabingwa.

Gerrard amekuwa nje ya ulingo wa ukocha tangu apigwe kalamu na Aston Villa mnamo Oktoba 2023.

Fowadi wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema, kiungo wa Wolves Ruben Neves na wanasoka watatu wa Chelsea – N’Golo Kante, Kalidou Koulibaly na Edouard Mendy ni miongoni mwa wachezaji kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambao wameyoyomea Saudi Arabia kumfuata Cristiano Ronaldo, wa hivi karibuni zaidi akiwa kiungo wa Inter Milan, Marcelo Brozovic aliyetua kambini mwa Al-Nassr.

Kocha wa Fulham, Marco Silva, amefichua kwamba amekataa ofa ya Sh3 bilioni ili kuwa mkufunzi wa kikosi cha Al-Hilal nchini Saudia.

Gerrard aliangika daluga zake kwenye ulingo wa soka mnamo 2016 na kikosi chake cha kwanza kunoa ni Rangers nchini Scotland.

Alipokezwa mikoba ya kikosi hicho mnamo 2018 na akakiongoza kuwaa taji la Ligi Kuu ya Scotland kwa mara ya kwanza baada ya miaka 10 mnamo 2020-21.

Gerrard baadaye aliteuliwa kuwa kocha wa Villa mnamo Novemba 2021 ila akapigwa kalamu baada ya kushinda mechi 13 pekee kutokana na 40 alizozisimamia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ingwe ya msimu ujao ni wembe – Shikanda

Wito watoto wanaoishi na ulemavu watunzwe vizuri

T L