• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Tarus, Bitok wataja vikosi vya Kenya vya voliboli kuwania ubingwa wa Bara Afrika

Tarus, Bitok wataja vikosi vya Kenya vya voliboli kuwania ubingwa wa Bara Afrika

Na AGNES MAKHANDIA

Makocha Gideon Tarus na Paul Bitok wametaja vikosi vya Kenya vitakavyowania Kombe la Afrika la voliboli la wanaume na wanawake jijini Kigali nchini Rwanda mnamo Septemba 5-16 na Septemba 10-20, mtawalia.

Tarus, ambaye ni kocha mkuu wa klabu ya GSU, pia anashikilia wadhifa huo katika timu ya taifa ya wanaume. Anachukua wadhifa huo kutoka kwa Moses Epoloto. Tarus atasaidiwa na kocha wa klabu ya wanaume ya Kenya Prisons David Lung’aho ambaye ni mkurugenzi wa kiufundi wa Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF) na kocha wa klabu ya KPA Sammy Mulinge.

Kocha wa klabu ya KDF Elisha Aliwa ambaye alikuwa mmoja wa maseta wazuri nchini enzi zake, ameteuliwa kuwa mmoja wa maafisa wa kusaidia katika mazoezi ya timu hiyo.

Tarus alikuwa katika benchi ya kiufundi ya wanaume mwaka 2016 chini ya kocha Gideon Chenje.

Wakati huo huo, KVF imejumuisha naibu kocha wa klabu ya kinadada ya Kenya Pipeline Esther Jepkosgei katika timu ya taifa ya kinadada kuhudumu kama afisa wa kusaidia timu hiyo mazoezini.

Bitok, ambaye anasalia kocha mkuu, ana manaibu wawili – Josp Barasa na Japheth Munala. Munala hakuwa katika timu iliyokuwa nchini Japan majuma machache yaliyopita kwa Olimpiki.

Mshambuliaji wa pembeni kushoto wa klabu ya Kenya Prisons Meldine Sande na mzuiaji wa kati wa klabu ya Kenya Pipeline Yvonne Sinaida wamejumuishwa katika kikosi cha watu 17 cha Malkia Strikers, huku seta wa klabu ya KCB Emmaculate Nekesa, ambaye alikuwa katika kikosi kilichojiandaa kwa Olimpiki, akikosa kuitwa kikosini.

Tarus ametaja kikosi cha wachezaji 18 wakiwemo maseta Brian Melly (GSU) na Kelvin Kipkosgei (Kenya Prisons), washambuliaji wa kati Jairus Kipkosgei (Kenya Prisons) na Simion Kipkorir (GSU) na libero Sam Juma (KPA) ambao walicheza mechi za kufuzu kushiriki michezo ya African Games za Zoni ya Tano mwaka 2019

Libero wa Equity Bank James Mutero na mshambuliaji wa pembeni kulia wa KPA Enock Mogeni, pia wamo kikosini.

Wachezaji watajika ambao hawakupata kuitwa kikosini ni washambuliaji Michael Chemos na Sila Kipruto na mzuiaji wa kati Rodgers Kipkirui, libero Noah Bett na mshambuliaji wa pembeni kushoto Bonfentry Mukekhe.

Kenya ilikamilisha ya nne kwenye zoni hiyo katika ambayo Misri iliibuka bingwa.

Kikosi cha wanaume: Brian Melly, Emmanuel Mwandari, Kelvin Kipkosgei, Sam Juma, James Mutero,Simion Kipkorir, Nelson Bitok, Shadrack Misiko, Lewis Ochieng, Benard Wechuli, Enock Mogeni, Kelvin Omuse, Cornelius Kiplagat, Joshua Kimaru, Aggrey Kibungei, Denis Omollo na Elphas Makuto.

Kikosi cha Malkia Strikers: Jane Wacu, Joy Lusenaka, Pamela Masaisai, Violet Makuto, Sharon Chepchumba, Mercy Moim, Carolyne Sirengo, Aggripina Kundu, Emmaculate Chemtai, Leonida Kasaya, Edith Wisa, Yvonne Sinaida, Gladys Ekaru,Lorine Chebet, Meldine Sande, Pamela Adhiambo na Elizabeth Wanyama.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali isidunishe uvaaji sare shuleni

Arsenal kutomkwamilia Aubameyang iwapo ataomba kuondoka...