Habari Mseto

Tahadhari Al Shabaab wanapanga shambulio

May 31st, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

MAGAIDI wa kundi la Al-Shabaab wanapanga kutekeleza mashambulio nchini hivi karibuni, Idara ya Polisi ilitoa tahadhari Jumatano.

Mkurugenzi wa mawasiliano katika idara hiyo, Bw Charles Owino, alisema idadi ya magaidi hao kwenye mpaka wa Kenya na Somalia imekuwa ikiongezeka na baadhi yao wanajaribu kuingia nchini kupitia Kaunti za Wajir, Mandera na Garissa.

“Idara ya Kitaifa ya Polisi ingependa kutoa ilani kwa wananchi wakae chonjo dhidi ya wale wanaopanga kuvuruga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kutekeleza mashambulio ya kigaidi,” akasema kwenye taarifa.

Hata hivyo, alihakikishia umma kwamba polisi wameimarisha usalama kote nchini na watafanikiwa kuzuia mashambulio yanayopangwa.

Idara hiyo ilitangaza tuzo la Sh3 milioni kwa yeyote atakayetoa habari zitakazosaidia kukamatwa kwa washukiwa watatu wa ugaidi ambao wanaaminika kuongoza kikundi kinachopanga kutatiza amani nchini.

Watatu hao ni Ibrahim Mohammed almaarufu Shariff Lin Kulul, Ahmed Dabar na Mumina Eroba ambaye ni mamake Ahmed. Kuna tuzo ya Sh1 milioni kwa atakayetoa habari zitakazosaidia kukamatwa kwa kila mmoja wao.

Ibrahim alisemekana kuwa amejificha katika eneo la Gedo nchini Somalia na amewahi kumtuma Ahmed kutafuta maeneo yanayoweza kushambuliwa katika Kaunti za Mandera na Wajir, yakiwemo maeneo yaliyo na watumishi wengi wa umma.