Habari

Tahadhari kuhusu Ebola

May 9th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI Jumatano ilitoa tahadhari baada ya mkurupuko wa maradhi hatari ya Ebola kutokea katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Waziri wa Afya, Bi Sicily Kariuki (pichani), alisema maafisa wa afya watachunguza wasafiri wote wanaoingia nchini kupitia sehemu za mpakani za Busia, Malaba na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

“Tumeweka vifaa vya kupima joto mwilini katika maeneo haya ili kutambua kama kiwango cha joto kitakuwa kimezidi kupita kiasi (kwa wasafiri),” akasema kwenye taarifa.

Kufikia jana, watu 17 walikuwa wamethibitishwa kufariki DRC baada ya kuambukizwa ugonjwa huo ambao huenea kwa kasi, na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) likasema limepeleka usaidizi ili kuzuia maambukizi kuenea zaidi.

Bi Kariuki aliongeza kuwa wizara yake imebuni Baraza la Tahadhari za Afya Kitaifa ambalo mojawapo ya majukumu yake itakuwa ni kuzuia magonjwa hatari kama vile Ebola kusambazwa nchini kutoka nchi za kigeni.

Hospitali zote nchini zinatarajiwa kupokea ilani kutoka kwa serikali ili kuweka mikakati maalumu itakayowezesha wahudumu wa matibabu kuwa macho na kutambua kama kuna maambukizi yoyote, na hatua zinazofaa kuchukuliwa.

Hata hivyo, Bi Kariuki alihakikishia Wakenya kwamba taifa hili lina utaalamu na uwezo wa kutosha kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.

“Wakenya wanafaa wawe watulivu kwani tumewahi kudhihirisha uwezo wetu wa kutambua na kuchukua hatua kwa haraka wakati wowote kunapokuwa na mkurupuko wa magonjwa,” akasema.

Mnamo 2015, Kenya ilikuwa miongoni mwa mataifa ambayo yalituma wahudumu wa afya Magharibi mwa Afrika wakati kulitokea mkurupuko mbaya zaidi wa Ebola ukanda huo.