Tahadhari kuhusu mafuriko mvua kubwa ikitarajiwa

Tahadhari kuhusu mafuriko mvua kubwa ikitarajiwa

NA COLLINS OMULO

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Kenya imeonya kuhusu kuzuka kwa mafuriko, maporomoko ya ardhi na mkurupuko wa maradhi yanayosambazwa kupitia maji.

Ilani hiyo imetolewa huku mvua kubwa ikitarajiwa kunyesha katika maeneo mengi nchini msimu wa masika ukianza.

Vile vile, idara hiyo imetahadharisha kuwa hali ya kiangazi inayoendelea Kaskazini mwa Kenya huenda ikaendelea huku eneo hilo likitarajiwa kupokea kiwango cha wastani cha mvua.

Aidha, imeonya kuhusu kuongezeka kwa visa vya homa ya dengue na chikungunya katika eneo la pwani.

Katika utabiri wake kuhusu msimu wa masika kati ya Machi na Aprili, idara hiyo ilisema mvua ya kawaida inatarajiwa katika maeneo ya juu ya Bonde la Ufa ikiwemo Nairobi, eneo la Ziwani na Kusini Mashariki.

Hata hivyo, mvua inayokaribia kiasi cha jumla inatarajiwa maeneo ya Kaskazini na Pwani ya Kenya.

Mvua hiyo kubwa huenda ikasababisha viwango vya maji kupanda katika Ziwa Victoria pamoja na maziwa katika Bonde la Ufa ikiwemo kusababisha mafuriko katika maeneo yanayoathirika zaidi kama vile Budalang’i na Nyando pamoja na Mto Tana na Athi River.

Maporomoko ya ardhi yanatarajiwa katika maeneo ya milimani yanayozingira Bonde la Ufa ya Mashariki na Magharibi hivyo kusababisha uharibifu wa miundomsingi ya barabara, madaraja na mijengo ya hali duni, hali ambayo huenda ikazua changamoto za usafiri, uharibifu wa mali na hata vifo.

“Mafuriko au maporomoko ya ardhi huenda yakasababisha watu na wanyama kufurushwa makwao ikiwemo kupoteza maisha, nafasi za kujipatia riziki na uharibifu wa mali. Barabara telezi na mwonekano hafifu wakati wa dhoruba za mvua huenda vilevile zikawa tishio kwa waendeshaji magari na abiria,” alisema Mkurugenzi wa KMD Stella Aura.

Kuna uwezekano mkuu wa radi kutokea hasa katika kaunti za Kisii, Kisumu, Nandi na Bungoma.

You can share this post!

Hofu ya vita Ukraine huku Urusi ikitengwa

Magoha aonya wakuu wa shule kuhusu karo

T L