Habari Mseto

Tahadhari mvua kubwa itanyesha kote nchini kwa wiki nzima

June 2nd, 2019 2 min read

Na COLLINS OMULO

IDARA ya utabiri wa hali ya anga nchini imetahadharisha kuwa kutakuwa na mvua kubwa katika maeneo mengi ya nchi kwa siku tano, huku msimu wa baridi ukibisha hodi.

Hali hiyo ya kati ya Juni 2 na 6 inatarajiwa kuathiri kaunti za Turkana, Samburu, West Pokot, Bomet, Kericho, Nandi, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Bungoma Kakamega, Vihiga, Busia, Nairobi, Nyeri, Murang’a, Kiambu, Embu, Tharaka Nithi, Meru, Kirinyaga, Narok, Nyandarua, Laikipia, Nakuru, Migori, Homa Bay, Siaya, Kisumu, Nyamira na Kisii.

“Wakazi katika maeneo yaliyotajwa wanashauriwa kuwa waangalifu kwa kuwa kunaweza kuwa na mafuriko. Watu waepuke kuendesha magari ama kutembea maeneo ambapo kuna maji mengi yanayosonga kwa kasi. Pia, watu wajiepushe na kukaa mahali wazi ama kujikinga chini ya miti kwani watahatarisha kupigwa radi,” mkurugenzi wa idara hiyo nchini Stella Aura akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa mwezi Juni utasalia kuwa mkavu katika maeneo mengi ya nchi, isipokuwa maeneo ya magharibi na pwani.

Maeneo ya Kericho, Kisumu, Kakamega, Kisii, Kitale, Eldoret pamoja na mengine kati mwa bonde la ufa kama Nakuru na Nyahururu yatapokea mvua ya kawaida, ambayo muda kwa muda inaweza kusambaa hadi Nairobi na eneo la kati.

Idara hiyo aidha imeonya wakazi katika maeneo ambapo ardhi hupasuka kama Murang’a kuwa waangalifu, pamoja na wale wa ambapo radi hupiga.

Hii ni baada ya radi kuua watu wanne eneo la Njoro, Nakuru Jumamosi jioni na kuwajeruhi wawili vibaya.

Aidha, maeneo ya Kwale, Kilifi, Lamu na sehemu za Tana River kusini yatapokea mvua ya kawaida, Nairobi na eneo la kati kukitarajiwa kushuhudiwa mawingu na baridi mchana na mvua chache asubuhi na alasiri, mwezi ukianza.

Lakini maeneo ya Wajir, Mandera, Garissa, Marsabit, Isiolo pamoja na Makueni, Kitui, Machakos, na Taita Taveta yatasalia kuwa makavu mwezi huu, idara hiyo ikasema.

Idara hiyo iliongeza kuwa mwezi uliopita, eneo la pwani kulishuhudiwa mvua kubwa, japo haikudumu kwa muda mrefu.

“Maeneo ya pwani, magharibi na kati yalishuhudia mvua kuwa kiasi. Ilidumu kwa siku chache lakini ilisababisha mafuriko katika maeneo fulani ya pwani,” akasema Bi Aura.

Alisema mvua ya msimu huo wa Machi-Aprili-Mei haikunyesha kwa utaratibu wa kawaida.

akisema nyingi ilishuhudiwa Aprili mwisho na Mei, japo maeneo mengi ya nchi Machi na muda mrefu Aprili yalikuwa kame.

“Mvua iliyoshuhudiwa katika sehemu nyingi za nchi kati ya Machi 1 na Mei 30 haikuwa ya kuridhisha,” akasema.