Habari Mseto

Tahadhari ya baridi kali kote nchini yatolewa

June 18th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

WAKENYA wametahadharishwa kujiandaa kwa baridi kali masaa ya asubuhi katika muda wa siku tatu zijazo huku kiwango cha joto kikitarajiwa kushuka hadi alama tatu katika baadhi ya semeu.

Mkurugenzi wa utabiri wa hali ya hewa Kenya, Peter Ambenje, alisema sehemu kadhaa za nchi zitakuwa na joto la kadri, mawingu na ukavu katika kipindi hicho.

Alisema nyakati za mchana katika siku chache zilizopita, kiwango cha joto kilishuka kote nchini isipokuwa Lamu huku kiwango cha joto kikiongezeka katika baadhi ya maeneo kama Nyahururu na Laikipia wiki jana. Hata hivyo, kilishuka maeneo ya Lodwar na Voi.

Kulingana na idara hiyo, baridi kali itashuhudiwa Nairobi, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi. Kiwango cha joto kitakuwa alama tatu na kikipanda zaidi kitakuwa 25 kwa kipimo cha Celsius.

Idara hiyo ilisema maeneo hayo yanayopatikana nyanda za juu za kati yatakuwa na mawingu nyakati za asubuhi na yanaweza kupata mvua sehemu chache na kupisha vipindi vya jua na manyunyu nyakati za alasiri.

Kaunti ambazo kwa kawaida huwa na joto kama vile Kitui, Makueni, Machakos na Taita Taveta pia zitakuwa na mawingu nyakati za asubuhi na vipindi ya jua alasiri.

Katika kaunti hizi kiwango cha joto kitashuka hadi alama saba katika kipimo cha Celsius.

Kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii na Nyamira zitakuwa na baridi japo haitakuwa kali kama maeneo mengine.

Katika kaunti za Ukanda wa pwani kiwango cha chini cha joto kitakuwa alama 19 na cha juu kitakuwa 30.