TAHARIRI: Afya ya uzazi kuhusu fistula itengewe pesa na mikakati

TAHARIRI: Afya ya uzazi kuhusu fistula itengewe pesa na mikakati

NA MHARIRI

JUMATATU ya leo ina umuhimu mkubwa kwa Kenya.

Ni siku ambapo Rais Uhuru Kenyatta anahudhuria mkutano wa 75 wa Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya afya nchini Uswisi.

Pia kila Mei 23, ulimwengu huendesha mwito wa kutokomeza ugonjwa wa fistula. Ni hali inayotokea pale mwanamke anaposhindwa kujizuia kutoa haja kubwa na ndogo.

Mara nyingi hili kujitokeza baada ya mwanamke mjamzito kuwa katika hali ya uchungu wa kujifungua kwa muda mrefu, kutokana na kichwa cha mtoto kushindwa kupita baada ya njia kuwa ndogo na mtoto kuwa mkubwa.

Uchungu huo wa muda mrefu husababisha tishu za uke, kibofu cha mkojo na njia ya haja kubwa kukandamizwa kati ya kichwa cha mtoto na nyonga za mwanamke.

Tundu hutokea kati ya uke na kibofu cha mkojo ama kati ya uke na njia ya haja kubwa, ambapo husababisha mwanamke kutoa haja kubwa au ndogo bila kujizuia kupitia uke wake.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kati ya wanawake 800 wamaokufa kila siku kutokana na kujifungua, 20 hufa kwa fistula.

Leo Jumatatu, ulimwengu unapoendeleza kampeni ya kutokomeza fistula, kauli mbiu ni “Angamiza Fistula Sasa: Wekeza katika Huduma Bora za Afya, Ziwezeshe Jamii!”

Wito huu ni muhimu sasa ambapo ulimwengu unakumbana na changamoto nyingi za kiafya.

Hapa nchini, tatizo hili la fistula lafaa kukabiliwa na wadau wote, hasa serikali na washirika wengine.

Wadau wanapokongamana jijini Geneva kwa kongamano la Baraza Kuu la Afya, wanapaswa kufuatilia kwa makini mapendekezo kuhusu mazingira bora ya kila mtu kupata huduma za afya.

Suala la kujiandaa na kukabili majanga pia ni muhimu, hasa wakati huu ambapo kumezuka mlipuko wa maradhi yanayohusishwa na nyani. Monkeypox inasemekana kuwa hatari mno.

Maradhi haya, kama ilivyokuwa homa ya Corona, yameanza nje ya Afrika lakini yanaweza kusambaa kwetu na kutuathiri kiafya na kiuchumi.

Viongozi wetu hawapaswi kusikiza hotuba kuhusu ufadhili wa afya bila ya kufuatilia. Wakati huu, mataifa mengi yamejiandaa kukabiliana na hali kama iliyoshuhudiwa mwaka 2020.

Kwetu Kenya, hata tutakapojiandaa kukabili maradhi ibuka, uzito mkubwa wafaa kuwa katika kuyakabili yale yaliyopo kwa sasa, ambayo yamechangia familia nyingi kudidimia katika umasikini.

Mbali na saratani, fistula ikabiliwe upesi kwa kuwa inaweza kutibika.

You can share this post!

Kalonzo kuamua leo ikiwa ama atawania au atarejea Azimio

Walimu waunga azma ya Wanga kuwania ugavana

T L