MakalaSiasa

TAHARIRI: Amina ana uwezo wa kuinua michezo

March 3rd, 2019 2 min read

NA MHARIRI

WIZARA ya Michezo nchini imekuwa na matatizo mengi katika miaka ya hivi majuzi hasa kutokana na ukosefu wa uongozi imara. Aghalabu mawaziri wanaoteuliwa kusimamia Wizara ya Michezo huwa wanafeli yamkini kutokana na ukosefu wa ari na utaalamu wa michezo.

Lakini baada ya kuteuliwa kwa Bi Amina Mohamed kama Waziri wa Michezo mnamo Ijumaa pana matumaini kuwa huenda mambo yakawa mazuri kuliko hali ilivyokuwa chini ya watangulizi wake.

Waziri anayeondoka Rashid Achesa alikuwa ameanza kuashiria kutindikiwa na maarifa ya kufufua sekta ya michezo, hali inayofaa kutumiwa na Amina kama funzo. Bi Amina alipata sifa kuu akiwa Waziri wa Masuala ya Kigeni’; tajriba anayotarajiwa kuirudufu katika spoti.

Changamoto kwa sasa ni tele katika fani ya michezo ambapo, kwa mfano, kikosi cha taifa cha raga ya wachezaji saba kila upande, Shujaa, kinashuhudia matokeo mabaya zaidi katika muda wa takribani muongo mmoja. Kwa sasa Shujaa inaning’inia katika eneo hatari duniani baada ya kushuhudia matokeo yasiyoridhisha hata kidogo.

Sababu kuu ya matokeo hayo ni uongozi duni katika shirikisho la mchezo huo nchini (KRU). Lakini pia pamesikika kuwa wachezaji hawalipwi wanavyostahili; wengine wakisemekana kupunguziwa mishahara.

Aidha, timu hiyo inatatizika kutokana na ukosefu wa ufadhili; jambo ambalo Bi Amina atahitajika kulishughulikia kwa dharura maadamu bila ufadhili mzuri kutoka kwa Serikali na mashirika ya kibiashara, timu au fani ya michezo haiwezi kupiga hatua ya maana.

Bi Amina anahitajika pia kumakinika wakati huu ambapo Harambee Stars inaelekea katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri.

Ni mwaka ambao tunatarajia timu hiyo ipite angaa hatua ya makundi kwani haijawahi kupata mafanikio hayo tangu kabumbu hiyo iasisiwe.

Je, timu hii inahitaji nini ndipo ifaulu katika fainali hizo? Serikali na wadhamini pamoja na wahisani waipe ufadhili wa kutosha kwa maandalizi mazuri; ikiwezekana ng’ambo ilivyopangwa, pamoja na fedha za kutosha kuwalipa wachezaji na benchi la ufundi.

Wala si timu hizi anazostahili kuzingatiwa na Waziri Amina, bali nyinginezo hasa zile zinazosaidia Kenya kujipa sifa katika mashindano ya kimataifa mfano wa riadha na voliboli.

Waziri huyo pia anatazamiwa kuangamiza ufisadi katika wizara hiyo, kuhakikisha kuna sera madhubuti za kuongoza michezo mbali na kuhimiza kudumishwa kwa sera hizo, pamoja na kustawisha miundomsingi ya michezo kama vile viwanja na ujenzi wa akademia nyingi za michezo.

Akademia hizo zitasaidia katika kuwapa wanamichezo wachanga wenye talanta msingi bora wa kufana katika siku zijazo.