Maoni

TAHARIRI: Bajeti ya kukopa itasalia mzigo kwa Wakenya

June 14th, 2024 2 min read

JANA Alhamisi Juni 13, 2024, serikali ya Kenya Kwanza kupitia kwa Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u iliwasilisha makadirio yake ya fedha ya 2024/2025.

Wananchi na viongozi wa matabaka mbalimbali walisubiri kwa hamu kujua mipango ya serikali.

Bila shaka, wengi walisubiri kuona iwapo serikali ina mipango yoyote ya kuhakikisha kwamba gharama ya maisha itapunguzwa.

Licha ya kwamba mwaka unaokamilika wa kifedha serikali haikuweza kutimiza malengo yake ya ushuru uliokusanywa ukizingatia bajeti ya mwaka uliopita, wengi walitarajia serikali ipunguze makadirio yake kutokana na nakisi ya mwaka unaokamilika.

Hata hivyo, Bajeti ya mwaka ujao wa kifedha imeongezwa.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba nyingi ya hela ambazo zinakusanywa na serikali kutoka kwa walipaushuru zitatumiwa katika ulipaji wa mikopo hasa ya kigeni.

Kwa mujibu wa takwimu, Kenya itatumia hadi asilimia 70 ya mapato yake kulipa madeni.

Kinaya kingine ni kwamba hadi asilimia 38 ya mapato ya kitaifa itatumiwa kulipa mishahara na gharama ya kuendeshea serikali.

Takwimu tulizonukuu hapo juu zina maana kwamba taifa litalazimika kukopa ili kuendesha miradi ya maendeleo.

Ukopaji huu wa kila mwaka ndio ambao umeongeza deni la kigeni kufikia Sh11 trilioni.

Fasiri nyepesi ya maisha ya Mkenya ni kwamba bila kukopa hawezi kuendesha maisha yake. Utegemezi huu wa mikopo ni sifa hatari.

Itakuwa ni fahari kubwa sana kwetu kama taifa iwapo utafika wakati ambapo itawezekana kujikusanyia mapato ambayo yanaweza kukidhi mahitaji ya taifa bila utegemezi wa mikopo.

Nakisi katika bajeti ndiyo imetugeuza kuwa ombaomba duniani.

Serikali iliyoko mamlakani ina jukumu la kuhakikisha kwamba inaongeza mapato yake kupitia njia mbalimbali ili kupunguza utegemezi.

Mathalan, tunatarajia serikali iweke mazingira bora ya uwekezaji ili kuwavutia wajasiria mali wengi waje kuwekeza humu nchini.

Hatua kama hii itabuni nafasi tele za ajira na hivyo kuwezesha raia wengi kujipatia riziki.

Zaidi ya hivyo, iwapo tutajitengenezea nyingi ya bidhaa tunazohitaji, basi tutapunguza utegemezi kwa bidhaa ya kuagiza.

Na iwapo tutawekeza vizuri katika sekta ya viwanda, basi tutaweza kuuza bidhaa zetu ng’ambo na hivyo kujipatia sarafu za kigeni.

Akiba nzuri ya sarafu za kigeni huwezesha kuboresha thamani ya sarafu yake na hivyo kukabili kwa urahisi mfumko wa gharama ya maisha kwani nchi humudu kuagizia bidhaa ambazo haina kwa njia rahisi.

Tukifanya hivi tutapunguza utegemezi wa mikopo kufadhili bajeti yetu ya kila mwaka.