Makala

TAHARIRI: Baraza la Kiswahili lisianze na kujikwaa

August 23rd, 2019 2 min read

Na MHARIRI

MPANGO wa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili Kenya umekuja wakati mwafaka ikizingatiwa kwamba kumekuwepo changamoto nyingi zinazoikumba lugha hiyo.

Baraza hilo litakapoanza kazi, litakuwa na kibarua kikubwa; hasa kuhusiana na mgawanyiko uliopo baina ya wadau wa Kiswahili.

Kuna habari kuwa tayari lipo jopo linalozunguka nchini kukusanya maoni ya wananchi kuhusu uundaji wa baraza lenyewe.

Lakini haijaeleweka wanachama wa jopo hilo ni akina nani na waliteuliwa kutumia vigezo vipi. Mara nyingi hapa Kenya, tumekuwa na tatizo la kuwagawa watu katika makundi.

Lipo kundi la watu ambao kweli wanakielewa Kiswahili lakini hawajasoma zaidi ya shahada ya digrii ya kwanza.

Wapo wanaokielewa na ni madaktari au maprofesa na kwenye kundi hilo pia wapo ambao hawajui lolote kuhusu Kiswahili, lakini kutokana na kuwa na ‘uprofesa’, wanajikita katika utafiti wa kubuni maneno yasiyokuwa na msingi wowote katika Uswahili wala Ubantu.

Huu mgawanyiko wa maprofesa na watu wasio wasomi ndio ugonjwa mkubwa ambao sharti utibiwe kwanza, kabla jopo halijapiga hatua. Kuna haja gani ya kuwa na Baraza la Kiswahili ambalo litakuwa linavutwa upande mmoja na ‘wanamapinduzi’ na upande mwingine ‘wahifadhina’?

Kutokana na ubabe uliopo, wadau wengi waliojitokeza wanaunda maneno kwa kutohoa yale ya Kiingereza pekee.

Kwani tutakuwa tukibuni maneno ya kukopa pekee? Sisi wenyewe hatuna akili za kuunda msamiati asili?

Kiswahili ni lugha iliyokubaliwa na Wakenya wengi mwaka 2010 wakaidhinisha katika Katiba kiwe lugha rasmi. Ni ajabu na jambo la kuudhi kuona hata wanasiasa wakikidunisha.

Majuzi, Seneta Maalum Dkt Agnes Zani alipojaribu kubuni neno linalomsimamia Spika, maseneta walianza kucheka na kuonekana hata hawajui kulitamka.

Ikiwa viongozi watakejeli lugha yao inayosomwa na wageni wengi na kuitumia katika shughuli zao za biashara, ina maana ule msemo wa mwacha mila ni mtumwa utatumiwa kutupigia mfano.

Mataifa ya Bara Asia yaliyopiga hatua kiteknolojia kama Japan, Korea, na Uchina, hayatumii Kiingereza.

Aina za magari yanayoundwa Japan, ni ushahidi tosha kuwa watu wanapozungumza lugha moja (ambayo si ya kukopa) wanaweza kupiga hatua kubwa.

Cha msingi zaidi, ni lazima wadau wa kila aina – wanahabari, walimu wa msingi na upili, wahadhiri, taasisi za utafiti, wazee wa miji ya Uswahilini na wengine, wawakilishwe vilivyo.