Makala

TAHARIRI: Boinnet anaondoka bila kutimiza mengi

March 12th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

KUKAMILIKA kwa kipindi cha kuhudumu Bw Joseph Boinett kama Inspekta Jenerali wa Polisi, kunatoa fursa kwa Wakenya kutafakari kuhusu wadhifa huo muhimu.

Bw Boinnet aliyechukua hatamu mnamo Desemba 2014 kutoka kwa David Kimaiyo ambaye wanatoka kaunti moja (Elgeyo Marakwet), anaondoka akiwa anaandamwa na kashfa tele.

Wakati huo aliahidi kupiga msasa huduma za polisi ambazo zilichukuliwa kuwa mbaya, hasa kutokana na madai ya kukithiri kwa ufisadi miongoni mwa maafisa wake. Polisi walikuwa mstari wa mbele kukaidi sheria na kutumia nguvu kupita kiasi.

Jana kwenye mtandao wake wa Twitter, Bw Boinnet alitaja yale anayodai kuwa ni ufanisi wake mkubwa. Miongoni mwa hayo ni kuleta mageuzi katika idara mbili za polisi.

Maafisa wa Polisi wa Utawala na wale wa kawaida sasa watakuwa kikosi kimoja, kinachovaa sare rangi moja. Sare hizo pia zimegeuzwa na kuwa za samawati.

Anasema polisi walipata vifaa vingi na vya kisasa, yakiwemo magari, ambayo anadai yamewasaidia maafisa hao kuitika mwito wa dharura kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kupitia mageuzi hayo, maafisa wa polisi sasa wana bima za maisha na Bw Boinnet anasema maafisa hao wanafanya kazi kwa kujitolea zaidi.

Pia anataja ufanisi wake mkuu kuwa nyongeza ya marupurupu ya nyumba kwa maafisa hao.

Hata hivyo, katika anayotaja kuwa ufanisi, yapo mengi ambayo bado hayajatekelezwa waka kufanywa kwa njia inayofaa.

Katika kuwapa polisi nyongeza hiyo ya marupurupu ya nyumba, Serikali pia iliwaondoa kutoka kwa nyumba za polisi. Inaeleweka kuwa nyumba hizo zilikuwa katika hali duni na zenye msongamano.

Polisi kuishi na umma ni vizuri kwa sababu watakuwa karibu na wananchi. Lakini pia serikali yapaswa kuangalia madhara ya wao kuwa miongoni mwa wahalifu.

Changamoto kubwa ambazo Bw Boinnet hakuzimudu na huenda hata mrithi wake akashindwa, ni kumaliza ufisadi katika idara ya polisi.

Utumiaji mbaya wa silaha lazima ukabiliwe vilivyo, baada ya kubainika kuwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, maafisa wa polisi kuwaua watu wengi ambao hawakuw ana hatia, wakiwemo watoto wadogo.

Ispekta Jenerali ajaye anapaswa kuwafanya maafisa wote watumikie wananchi bila kuegemea mirengo ya kisiasa.