Makala

TAHARIRI: CBK ifuatilie makini utendakazi wa benki

January 9th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

WAKATI huu ambapo wazazi wanarejesha watoto wao shuleni au kuwasajili wengine katika shule za upili, benki zinapaswa kuwarahisishia kibarua cha kulipa karo.

Wazazi wengi wanaendelea kuhangaika kwenye maduka ya sare, vitabu na vifaa vingine vya shule. Kwa hivyo kazi yao si kupanga laini kwenye benki pekee ili kusubiri kulipa karo.

Katika harakati za kulipa pesa, imegundulika kuwa baadhi ya benki zinawahangaisha wazazi kwa kuwapigisha foleni na kisha baadaye kuwalekeza kwingine.

Kwa mfano, kuna wazazi ambao walipanga mistari mirefu nje ya benki na walipofika sehemu za kufanyia malipo, wakaagizwa waende kulipa kwa maajenti.

Benki zikiwa taasisi zinazohudumia wateja, zinapaswa kuwa wa maafisa wa uhusiano mwema. Watu hao, kazi yao yafaa kuwa ya kuwauliza wateja – kila mmoja kama mtu binafsi – kuhusu huduma wanazohitaji na aina gani ya fomu za kuchukua. Pia, yafaa wawaelekeze mahali pa kuanzia na kadhalika.

Kuna benki ambazo japo zinafanya haya, zinawatumia walinzi ambao wakati mwingine wanakuwa wajeuri, wakali au wasioelewa hisia za watu.

Malipo ya karo mara nyingi huwa yanafanywa kulingana na maagizo kutoka kwa shule husika. Kuna shule ambazo wasimamizi wanakataa risiti zilizopatikana kutoka kwa maajenti. Benki inapoelezwa na mteja kuwa angependa kulipa kwa keshia wa benki badala ya ajenti, zinafaa kusheshimu maelezo hayo.

Wahudumu katika benki ni wafanyikazi kama wafanyikazi wa sekta nyingine na wanasimamiwa na kuongozwa na kanuni maalum. Mojawapo ya kanuni kuu katika taasisi zote zinazohudumia wateja, ni kaulimbiu kuwa ‘mteja ni mfalme’.

Mteja ana haki ya kusikizwa na kuhudumiwa kulingana na mahitaji yake. Mhudumu wa benki anachoweza kufanya ni kumshauri mteja kuhusu njia bora ya kuhudumiwa, na wala si kumpuuza na kumshurutisha afanye kinyume na matakwa au katika suala la karo, maagizo ya shule.

Benki Kuu ya Kenya inayosimamia utendakazi wa benki, yapaswa kupeleleza jinsi baadhi ya benki zinavyotumia maajenti kuhangaisha wateja. Ni jambo zuri kuwa maajenti wanarahisisha upatikanaji wa huduma za benki hata mitaani. Lakini iwapo meja atasema kuwa ana maagizo alipe pesa kwa keshia wa benki pekee, hili si jambo la kufanyiwa mzaha.