Makala

TAHARIRI: Wizara ya Afya izuie vifo hivi

July 15th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

JUMANNE iliripotiwa katika vyombo vya habari kuwa kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya kiko juu zaidi ikilinganishwa na mataifa mengine ya ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Kufikia jana Jumanne, Kenya ilikuwa imepoteza raia 202 kati ya jumla ya maambukizi 10,791 hii ikiwa karibu asilimia 2 ya wagonjwa.

Mnamo Jumatatu, taifa hili lilirekodi idadi kubwa zaidi ya vifo kwa siku moja ambavyo viligonga 12. Vifo hivyo vya Jumanne yamkini vinatoa dalili ya jinsi mambo yatakavyokuwa katika siku zijazo nchini.

Huku Kenya ikirekodi idadi hiyo kubwa, mataifa kama vile Uganda na Rwanda, yamesajili vifo vichache zaidi. Kati ya jumla ya maambukizi 1,378 Rwanda imepoteza raia wanne pekee huku Uganda yenye maambukizi 1,040 ikiwa haijapoteza raia yeyote.

Kihisabati, Rwanda imepoteza asilimia 0.4 pekee huku Uganda ikiwa imepoteza asilimia 0! Tanzania na Burundi si mataifa mwafaka ya kutumia kama kigezo kwa sababu pamekuwa na tashtiti kuhusu jinsi yanavyotangaza maambukizi yayo kwa umma na kimataifa.

Unaporudi nyuma na kufanya ulinganisho, Kenya ilikuwa na zaidi ya vifo 50 wakati ikiwa na maambukizi yapatayo 1,000

Hiyo inamaanisha kuwa wakati huo taifa hili lilikuwa likipoteza asilimia tano ya walioambukizwa na virusi hivyo vya corona.

Japo kutokana na ulinganisho huo Kenya imepiga hatua na kufaulu kudhibiti kiwango cha vifo, bado pana haja ya kujizatiti zaidi ili taifa hili lisipoteze raia wengi wakati maambukizi ya ugonjwa huu yatakapofikia kilele.

Naam, yapo mataifa yanayopoteza idadi kubwa ya raia wake kuliko hii ya Kenya, lakini si vizuri kusikia kuwa Kenya inaongoza kwa vifo katika ukanda huu.

Si katika ukanda tu, kadhalika, Kenya imo miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayopoteza raia wake wengi kwa siku.

Hivyo basi, pana haja ya Serikali hasa kupitia kwa Wizara ya Afya kuchunguza sababu za taifa hili kuendelea kuongoza kwa mauti haya.

Ikizingatiwa kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa yanayojivunia sekta bora zaidi ya afya, inakuwa kinaya kuwa inashindwa kuzuia vifo vingi vya raia wake kutokana na corona.

Yamkini madaktari wetu na wahudumu wa kiafya wanalala kazini? Sharti uchunguzi ufanywe kujua ni kitu gani tusichofanya jinsi inavyostahili.