Makala

TAHARIRI: Covid: Tusingoje serikali ituokoe

November 5th, 2020 1 min read

KITENGO CHA UHARIRI

WANANCHI wengi huenda walitarajia serikali ingerudisha masharti makali ya kupambana na virusi vya corona jana Jumatano.

Kwa kuzingatia midahalo katika jamii ikiwemo mitandaoni, wengi walitarajia kwamba kutokana na ongezeko la kasi la maambukizi katika mwezi mmoja uliopita, Rais Uhuru Kenyatta angerudisha kanuni zilizokuwepo mwanzoni mwa janga hili nchini.

Kanuni hizo ni kama vile kufunga maeneo kunako maambukizi mengi, kufunga shule kwa wanafunzi ambao walirejea, kufunga sehemu za burudani zilizofunguliwa kama vile baa, miongoni mwa mengine.

Katika hotuba yake, ilibainika wazi kwamba Rais alijiepusha kutangaza hatua ambazo zingedhuru zaidi hali ya maisha ya wananchi.

Hatua hiyo inaridhisha kiasi cha haja kwa sababu kuna wengi ambao wakati kanuni zilipolegezwa, walianza kufufua hali zao za kimaisha zilizokuwa zimedorora. Kwa msingi huu, kurudisha masharti makali kungedhuru raia kwa mara nyingine.

Tulipofikia sasa inafaa kila mwananchi ajue kwamba sheria pekee hazitoshi kuepusha maambukizi ya corona. Tumekumbushwa kila mara kwamba virusi hivyo havina miguu wala maarifa, bali ni sisi wenyewe tunavisaidia kuenea tunapopuuza mawaidha ya wataalamu wa afya.

Inashangaza kuwa kufikia sasa, bado kuna baadhi yetu wanaotilia shaka uwepo wa corona na maangamizi ambayo ugonjwa wa Covid-19 husababisha kwa binadamu.

Uepushaji wa maambukizi ni jukumu la kila mmoja wetu. Haijalishi kile ambacho wanasiasa wanafanya, kwani raia atakapotaabika hakuna mwanasiasa atakuja kumsaidia. Tusitazame kile viongozi wanafanya kisha tuwafuate kikondoo, bali tutii mawaidha ya wataalamu.

Huenda wewe ukaponea utakapoambukizwa, kwa vile u buheri wa afya na pengine kijana, lakini kumbuka utepetevu wako katika vita hivi unaweza kusababisha vifo vingi vya watu ambao utatagusana nao.

Kwa miezi michache sasa, serikali imeonyesha itajihusisha zaidi katika kufufua uchumi itakapoweka masharti ya kuepusha maambukizi ya corona.

Kwa hivyo, ni wajibu wa kila mtu sasa kujilinda mwenyewe na wapendwa wake badala ya kusubiri kuona kile kitakachofanywa na serikali.