Makala

TAHARIRI: DCI isafishe ufisadi katika soka ya Kenya

May 23rd, 2020 2 min read

Na MHARIRI

MNAMO Alhamisi wiki hii, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa alihojiwa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi ya kesi za Jinai (DCI) kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya fedha katika ofisi yake.

Mwendwa alifika katika afisi za DCI akiandamana na Naibu wake Doris Petra na Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno.

Alihojiwa kuhusu namna FKF ilivyotumia Sh244m zilizotolewa na serikali mwaka uliopita kwa minajili ya kuiandaa timu ya taifa ya Harambee Stars kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizofanyika nchini Misri.

Alitakiwa pia kuelezea jinsi ambavyo baadhi ya maafisa wa FKF, yeye akiwemo, walivyojipa marupurupu ya hadi Sh50,000 kwa siku wakati wa kampeni za AFCON nchini Misri.

Kuhojiwa kwa Mwendwa kulifanyika siku chache baada ya nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama, kuthibitisha kwamba wanasoka wa timu ya taifa ya Kenya bado hawajalipwa bonasi walizoahidiwa kwa ushindi wa 3-2 waliousajili dhidi ya Tanzania katika AFCON 2019.

Jingine ambalo Mwendwa alitakiwa kufafanua ni kuhusu hatima ya basi la Sh125 milioni ambalo lilinunuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kwa minajili ya kuchangia maendeleo ya soka ya Kenya.

Uozo ambao DCI inalenga kufichua katika FKF kabla ya mashtaka kufunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) unafanyika wakati ambapo soka inakabiliwa na suitafahamu baada ya uchaguzi wa FKF kufutiliwa mbali mara mbili na Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT).

FKF inachunguzwa pia kwa kushindwa kuwalipa makocha wa zamani wa Harambee Stars Adel Amrouche, Bobby Williamson na Sebastien Migne ambao kwa pamoja, wanadai kima cha Sh170 milioni.

Haya si matukio ya kwanza kuwahi kuaibisha Kenya katika medani ya kimataifa. Pamewahi kutokea mipangilio mibaya na nyendo zisizofaa mara nyingi Harambee Stars inapoenda kuchezea nje ya nchi. Halijawahi kuwa jambo geni kwa wanasoka wa Harambee Stars kuzuiliwa hotelini kwa kushindwa kugharimia malaji na malazi, au hata kukwama njiani baada ya ndege kukosa kulipiwa kwa wakati unaofaa huku vinara wa soka wakijishaua kwa matumbo yasiyoshiba!

Sharti hatua kali zichukuliwe kuzima ufisadi hasa ndani ya FKF na Wizara ya Michezo inafaa ihakikishe kuwa kuna mipango mizuri inayofanywa mapema kabla ya timu yoyote ya taifa kuondoka kuenda kuwajibikia taifa ugenini au FKF kuajiri kocha yeyote mwingine wa Harambee Stars.