TAHARIRI: EAC waungane kukabili corona

TAHARIRI: EAC waungane kukabili corona

Na MHARIRI

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kufunga mipaka ya Kenya na nchi za Tanzania na Somalia mnamo Jumamosi, ni jambo zuri, linaloonyesha jinsi serikali inayajali maisha ya Wakenya.

Serikali ilichukua hatua hiyo baada ya kubainika kuwa maeneo ya mipakani yameibukia kuwa vitovu vipya vya maambukizi ya virusi hivyo.

Bila shaka, uwepo wa virusi unaendelea kuitikisa Kenya na dunia nzima, hasa baada ya visa 57 zaidi kuthibitishwa jana, hilo likifikisha idadi ya watu walioambukizwa nchini kuwa 887.

Hata hivyo, imeibuka kwamba huenda hatua ya Kenya ikazua taharuki kati yake na nchi hizo mbili, kwani bado haijabainika ikiwa kulikuwa na mashauriano kati ya marais husika.

Ingawa serikali haikueleza utaratibu iliyofuata katika kufikia hatua hiyo, ni muhimu kwa Rais Kenyatta kujitokeza wazi kueleza ikiwa alishauriana na marais John Magufuli (Tanzania) na Mohamed Farmajo (Somalia).

Hii ni kwa kuwa uamuzi huo una athari kwa raia wa mataifa hayo matatu. Bila shaka, si mara moja ambapo tumeona taharuki zikizuka, hasa kati ya Kenya na Tanzania, kuhusu masuala yanayohusu ushirikiano wa kibiashara.

Kwa mara kadha, imeripotiwa kuwa maafisa wa Tanzania wametwaa bidhaa za wafanyabiashara kutoka Kenya na kuziharibu au hata kuzichoma, kwa kisingizio cha kuingia nchini humo bila kufuata taratibu za kisheria zifaazo.

Ni vitendo ambavyo vilizidisha uhasama kati ya mataifa hayo mawili, hali iliyowalazimu marais Kenyatta na Magufuli kukutana ili kusuluhisha tofauti hizo.

Uwepo wa corona unaonekana kuturudisha tulikokuwa. Tanzania imelaumiwa na nchi kadhaa, ikiwemo Amerika, kwa hatua inazochukua katika kukabili janga hilo.

Viongozi kadha pia wamemlaumu Rais Magufuli kwamba, hachukui hatua zifaazo kuiwezesha nchi yake kukabili virusi, ndipo visa vinaongezeka sana huko.

Ikizingatiwa kuwa Kenya na Tanzania ni majirani na wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuna haja ya viongozi wake kushirikiana ili kuimarisha mikakati ya kukabili janga hili.

Kuelekezeana lawama hakufai kwa sasa, kwani kando na corona, kuna masuala mengi muhimu yatakayohitaji ushirikiano wa mataifa hayo.

You can share this post!

AMROUCHE: Kenya yakodolea macho marufuku kutoka kwa Fifa

WASONGA: Machifu wasikwamishe mpango wa usafi mitaani

adminleo