TAHARIRI: Elimu si jukumu la serikali pekee

TAHARIRI: Elimu si jukumu la serikali pekee

KITENGO CHA UHARIRI

SHULE zinapofungwa wiki hii, wanafunzi watatarajiwa kupumzika kwa wiki mbili pekee na kurejea shuleni kabla ya mwisho wa mwezi.

Mapumziko haya yatawapa nafasi ya kujiandaa kujiunga na madarasa mapya. Kwa mara ya kwanza wanafunzi wa Darasa la Nne chini ya mfumo mpya wa CBC, watajiunga na Darasa la Tano. Watoto hao wamekuwa nyumbani tangu mwezi Machi.

Aidha, maelfu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa Darasa la Nane mwezi Machi wanajiunga na Kidato cha Kwanza mwanzoni mwa Agosti. Kujazana wanafunzi kunawalazimu walimu wakuu wa shule za upili kuweka mikakati ya kupunguza msongamano.

Tume ya kuajiri walimu (TSC) imeahidi kuajiri walimu wa ziada kukabiliana na ongezeko hilo la wanafunzi.

Wikendi hii, viongozi wa maeneo ya Kaskazini mwa nchi walimlalamikia Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha. Walilalama kwamba kumekuwa na ubaguzi katika uajiri wa walimu unapofanywa na TSC.

Tume hiyo imekuwa ikipeleka walimu wachache katika kaunti za Garissa, Wajir na Mandera. Isitoshe, kanuni za watu kujiunga na vyuo vya walimu zimewazuia wakazi wengi kuwa walimu. Kwa mfano masomo yanayotakikana pamoja na gredi kupandishwa, yaonekana ni masharti yasiyozingatia upekee wa maeneo yanayochukuliwa kuwa kame au yaliyotengwa.

Wenyeji wangefaa zaidi kufundisha watoto wao, kwa kuwa wanaelewa maeneo hayo na huenda wasiwe na mahitaji mengi kama watu wa kutoka nje.

Haki ya elimu ni mojawapo ya haki za kimsingi kwenye katiba yetu. Hili linaweza kutekelezwa vizuri iwapo TSC itapeleka walimu wa kutosha katika kila pembe ya nchi.

Lakini wakati vingozi wa Kaskazini wakilaumu TSC, wanapaswa kuketi chini na wenzao wa utawala na wakazi kwa jumla. Wajadiliane kuhusu umuhimu wa usalama. Kila mtu anapoambiwa anatumwa kufundisha Garissa, Wajir au Mandera hukataa, anapokumbuka matukio ambapo magaidi wamekuwa wakishambulia walimu wa kutoka nje ya eneo hilo.

Magaidi hao wanaweza kuzuiwa kushambulia watu, ikiwa wakazi na viongozi watakuwa wakiwapasha habari maafisa usalama. Kuwaficha na kuwaruhusu waenbdeleze uhalifu, ni kujitenga kiuchumi na kimaendeleo.

You can share this post!

Ramaphosa aomba utulivu wafuasi wa Zuma wakizua fujo

WARUI: Nafasi 10,000 za kazi TSC ilitangaza ni chache mno