Makala

TAHARIRI: FKF isaidie klabu kupata udhamini

November 28th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

MNAMO Alhamisi, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) liliingia mkataba na kampuni ya kupeperusha matangazo ya runinga ya StarTimes ambayo ilikabadhiwa haki za kupeperusha mechi zote za Ligi Kuu ya Kenya.

Hii ni hatua moja ambayo japo si kubwa sana, ni ya maana na inayopaswa kuwafungua macho viongozi wa kandanda nchini kutafuta washirika zaidi watakaohakikisha kuwa ligi kuu, ligi za daraja za chini pamoja na klabu zinapata udhamini wa kutosha.

Shirika hilo ambalo huuza ving’amuzi vya kuwezesha matangazo ya runinga na redio, limekubali kutoa Sh110 milioni kila mwaka kwa miaka saba kuhakikisha kuwa mechi za kabumbu ya Ligi Kuu (KPL) zinapeperushwa kupitia kwa runinga ya KTN.

Hatua hiyo inasaidia kuziba pengo lililoachwa na SuperSport iliyojiondoa yapata miaka miwili iliyopita.

Hata hivyo, itakuwa bora zaidi iwapo wadau wa kandanda watashirikiana kuzitafutia klabu zetu udhamini kutoka hasa kwa mashirika ya kibiashara.

Nyingi ya klabu zinazosakata ligi kuu zinatatizika sana kifedha hasa kutokana na makali ya janga la corona pamoja na ukosefu wa udhamini.

Naam, ni habari nzuri kuwa kampuni ya kamari ya spoti ya BetKing ilishakubali kudhamini klabu za Kenya pamoja na ligi kuu kwa kima cha Sh1.2 bilioni kwa miaka mitano.

Unapozigawa pesa hizo katika kiwango cha mwaka mmoja, udhamini huo unakuwa Sh240 milioni. Kwa hakika klabu 18 zinapogawana pesa hizo, kila moja inapata Sh13.3 milioni.

Japo kiasi hicho ni kizuri maadamu kitaokoa timu nyingi dhidi ya kuzama katika ufukara jinsi ilivyoshuhudiwa katika msimu uliopita ambao ulikatizwa na corona, gharama za klabu hushinda hela hizo kwa mwaka.

Hii ina maana kuwa, klabu zetu zinahitaji ufadhili zaidi ili kupiga jeki ufanisi wa soka hasa ya kiwango cha kitaifa mathalani KPL.

Ingawa jukumu kubwa la kutafuta ufadhili linabaki mikononi mwa klabu zenyewe, pana nafasi kubwa ya klabu hizo kufanikiwa kupata udhamini iwapo shirikisho la FKF litazisaidia timu hizo zetu kuupata udhamini.

Zipo kampuni nyingi za kibiashara humu nchini ambazo ninaamini zikishawishiwa vizuri, zitaanza kudhamini klabu zetu.