Makala

TAHARIRI: Ghasia za kisiasa zikomeshwe upesi

October 5th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

TUKIO la Jumapili ambapo watu wawili waliuawa kwenye ghasia za mkutano wa kisiasa mjini Kenol, Kaunti ya Murang’a ni dalili mbaya za jinsi nchi hii inavyoweza kutumbukia kwenye fujo, iwapo hatutachukua hatua za haraka.

Fujo hizo zilijiri baada ya wiki ya malumbano makali na vitisho kati ya wafuasi wa Dkt Ruto na wale wa Rais Uhuru Kenyatta, yaliyoanza naibu rais alipovamia makao makuu ya Jubilee akiwa na washirika wake wa kisiasa.

Inasemekana kuwa mmoja wa waliouawa alikuwa miongoni mwa kundi la vijana waliokuwa wakinuia kuvuruga hafla ya Dkt Ruto katika kanisa la AIPCA Kenol.

Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na mbunge wa Kandara, Bi AliceWahome walidai kwamba vijana wa mrengo wa Kieleweke wa chama cha Jubilee waliwasili mjini Kenol kuanzia saa kumi na moja alfajiri wakiimba nyimbo za kumsifu Rais Uhuru Kenyatta.

Wafuasi wa Dkt Ruto nao walikusanyika haraka na mji wa Kenol ukabadilika kuwa uwanja wa vita. Baadaye Seneta wa Murang’a Irungu Kangata alisema fujo hizo hazingetokea kama wafuasi wa Dkt Ruto hawangeanza siasa za mapema.

Matamshi haya hayafai kutolewa na kiongozi mwenye hadhi ya Kiranja wa Bunge la Seneti. Yanaweza kutafsiriwa kuwa kweli, ghasia hizo zilipangwa.

Katika kuonyeshana ubabe wa kisiasa, wanaoumia au kuuawa ni wananchi wasiokuwa na hatia. Vijana, kwa kuwa na matumaini ya kupata pesa kutoka kwa wanasiasa, hujazana kwenye mikutano hii.

Kwa hivyo, ipo haja kwa maafisa wa usalama kuwa macho na kuhakikisha kwamba wanasiasa hawatumii wahuni kusababisha umwagikaji wa damu.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai alisema ameunda jopo la wapelelezi kuchunguza kilichosababisha fujo hizo na kuuawa kwa wanaume wawili.

Ni matumaini ya Wakenya wote kwamba jopo hilo litatekeleza majukumu yake bila ya kuegemea upande wowote wa kisiasa. Kuchunguza pekee hakutoshi.

Watakaogunduliwa kuhusika na ghasia hizo yafaa wakamatwe na kushtakiwa, kukiwa na ushahidi wa kutosha kuwezesha korti kuwatumia kama mfano.

Bila hivyo, huenda kampeni za kisiasa za BBI na zile za Uchaguzi Mkuu wa 2022 zikasababisha machafuko mabaya zaidi ya yale ya 2007.