Makala

TAHARIRI: ‘Ghost’ ajiepushe na dosari za awali

October 24th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

ULIKUWA mwaka wa 2004 jijini Tunis nchini Tunisia.

Macho yote ya Wakenya yalikuwa yameelekezwa kwa fainali za Kombe la Afrika zilizokuwa zinaandaliwa nchini humo.

Kenya ilikuwa imepangwa kwenye kundi moja na majabali Senegal waliokuwa wamefika hatua ya robo fainali katika fainali za Kombe la Dunia mnamo 2002, pamoja na majabari wengine Mali, na Burkina Faso.

Palikuwapo matumaini japo finyu ya Harambee Stars kupiga hatua katika fainali hizo. Ingawa fursa ya Kenya kupiga hatua hiyo ilikuwa ndogo, wachanganuzi wengi walionelea kuwa taifa hili lingefanikiwa katika hilo iwapo kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee angecheza ‘karata’ zake vyema.

Kenya ilianza kupoteza mechi zake hata kabla ya kipenga kulia pale kocha Ghost alipofanya uteuzi mbaya wa kikosi cha kwanza kwa kujumuisha wanasoka wadhaifu hasa katika safu ya ulinzi pamoja na kuwapanga kikosini wanasoka wasioelewana vizuri hasa kwenye uvamizi.

Wadadisi wa masuala ya soka walibaini udhaifu wa kocha huyo pale alipokosa kumjumuisha John Baraza asaidiane na Dennis Oliech. Katika mechi za kufuzu, ilikuwa imebainika kuwa Harambee haitambi bila Baraza kuchezeshwa kwa pamoja na Oliech, maadamu wawili hao walikuwa wanaelewana barabara uwanjani.

Dosari hiyo iliinyima Kenya ushindi au angaa sare kwenye mechi zake mbili za mwanzo dhidi ya Mali na Senegal.

Uchanganuzi wa wadadisi ulionekana kuwa sahihi pale Baraza alipoingizwa kwa wakati mmoja na Oliech kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Burkina Faso. Kenya ilishinda mechi hiyo kwa mabao 3-0.

Nimetanguliza kumbukumbu hii kwa kuwa si tu kocha Ghost aliyewahi kufanya kosa hilo bali wenzake kadhaa akiwemo Sebastie Migne katika fainali za Afrika za mwaka jana nchini Misri.

Kocha Migne alianza kukosea katika uteuzi wa kikosi kilichoelekea kwenye fainali hizo alipowaacha wanasoka wenye tajriba mbali na kutumia mbinu ya kujikinga hasa Harambee ilipochuana na na Algeria na Senegal. Ilirambishwa mabao 3-0 kwenye kila mojawapo ya mechi hizo.

Udhaifu huu kwa kiasi fulani ulichangia katika kutimuliwa kwa Migne kisha Francis Kimanzi akateuliwa kumrithi.

Kabla ya Kimanzi kumaliza mwaka mmoja kama mkufunzi wa Stars, ameng’olewa ghafla na nafasi yake kutwaliwa na Ghost anayetarajiwa kuongoza kikosi hicho cha taifa kufuzu kwa fainali zijazo za Afrika na Kombe la Dunia.

Ili kuepuka ghadhabu za Wakenya wakiongozwa na Shirikisho la Soka nchini (FKF), kocha huyo mpya ajifunze kutokana na makosa ya hapo awali.