Makala

TAHARIRI: Habari kuhusu Ebola zisiwe za kuzua hofu

June 18th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

KUNA haja kubwa kwa maafisa katika Wizara ya Afya kuwa katika hali ya tahadhari wakati huu ambapo kumekuwa na mkurupuko wa maradhi hatari ya Ebola katika mataifa jirani ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Vile vile, wataalamu hao wanapaswa kudhibiti mawasiliano kuhusiana na habari za kupotosha kuhusu maambukizi ya maradhi hayo hatari.

Kuna maradhi mengi ambayo yana dalili zinazofanana. Kwa mfano, ni vigumu kubainisha iwapo mgonjwa anaugua malaria au homa ya matumbo kwa sababu dalili za magonjwa hayo mawili zinafana kwa kiwango kikubwa.

Ni kwa mintaarafu hii tunahimiza maafisa wa afya katika Hospitali ya Kericho na nyinginezo za umma kuwa makini zaidi na kuthibitisha visa vya maambukizi ya maradhi kama hayo kabla ya kusambaza habari hizo kwa umma.

Isitoshe, kuna haja ya wizara ya afya kuanzisha kampeni ya kitaifa kuhamasisha raia kuhusu maradhi hayo ambayo dalili zake za awali ni mafua, uchovu, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa na maumivu ya koo.

Maafisa wa usalama katika sehemu za mpakani na wale wa uhamiaji wanapasa, kwa moyo wa uzalendo, kuwa macho na kushirikiana kikamilifu na wataalamu wa afya kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini wanakaguliwa kikamilifu.

Sehemu nyingi za mipakani hazina maafisa wa uhamiaji na inakuwa rahisi kwa wageni kuingia nchini bila tatizo. Yamkini, kwa sasa wale wanaochunguzwa ni wale wanaotumia ndege kwa usafiri. Je, wale wanaoingia Kenya kupitia maeneo mengine ya mpakani kama vile vile Busia na kwingineko watadhibitiwaje?

Tunachosema hapa ni kwamba, maradhi ya Ebola si ngano, yapo na yanaua kwa kasi mno. Yameua wengi katika DRC na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Serikali ilichukua hatua nzuri kuwapeleka wataalamu wenye tajiriba ya kutosha kwenye viwanja vyetu vya ndege kukabiliana na maradhi hayo. Wataalamu hao waliwahi kujumuika na wenzao kutoka kwingineko duniani kupambana na maradhi hayo nchini Liberia, Sierra Leone na DRC.

Wito wetu ni kwa raia wenzetu kuhakikisha wanawapasha habari wataalamu wa afya endapo watashuhudia kisa wanachoshuku ni cha maambukizi ya Ebola.

Ni kwa kushirikiana kama nchi tunaweza kuzuia maradhi hayo hatari kusambaa nchini mwetu.