Makala

TAHARIRI: Haifai hela za shule kucheleweshwa

January 25th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

Serikali ilitoa ahadi ya kutoa elimu bila malipo kwa kila mtoto humu nchini kwa shule za msingi na sekondari.

Huku serikali ikipongezwa kwa hatua hii, ni jambo la kusikitisha kuona jinsi utekelezaji wa mradi huu unavyoendelea kuvunja wengi moyo. Kwa muda wa miaka kadha sasa, wadau wa kutoa ufadhili huu wamekuwa wakichelewesha fedha hizi kufika shuleni.

Kwa sasa, shule za umma zimekwama kifedha na haziwezi kuendeleza mipango na miradi yao muhimu kwa kukosa pesa.

Kwa hakika wasimamizi wa shule za umma za msingi na za upili walikuwa wakitarajia kupokea ufadhili huu mwezi uliopita kabla ya shule kufunguliwa kama serikali ilivyokuwa imeahidi.

Kinyume cha matarajio yao, wakuu hao wamejipata katika njia panda wiki ya tatu baada ya watoto kuingia shuleni.

Baadhi ya shule nyingi nchini haziwezi kununua vitabu, kalamu, chaki na vifaa vingi vingine muhimu vya kufanikisha shughuli za ufunzaji.

Ikumbukwe kwamba, ni serikali yenyewe inayopanga mitaala na ratiba za kufunga na kufungua shule na bila shaka mipango hii ya inafaa kwenda sambamba na utoaji wa fedha za shule. Hili lisilotekelezwa ni lazima kuwe na mkwaruzano wa mipangilio ya masomo ya taasisi hizi.

Utata huu unapotokea, ni dhahiri kwamba ubora wa elimu unaathirika pakubwa kiasi cha kusababisha utovu wa nidhamu na hata matokeo mabaya ya mtihani.

Ni sharti serikali ifahamu kwamba kwamba, haki ya kila mwanafunzi kupata elimu bora inalindwa na katiba ya nchi hii. Fauka ya hayo, kila mwanafunzi ana haki ya kibinadamu kupata elimu.

Kwa kuzingatia mantiki hii, ni sharti maafisa husika wa serikali wafahamu kuwa wanafaa kutoa za hela za kugharamia elimu wakati ufaao bila kuchelewa.

Pili, waelewe kwamba, ili kufikia sera ambazo serikali imetoa ni jukumu lao kuzifanikisha bila kusita.

Agizo la serikali kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa KCPE mwaka uliopita watajiunga na shule za upili nchini hautatekelezwa kikamilifu endapo fedha za kufadhili elimu zitaendela kuchelewa hivi.

Suala la waziri wa Fedha Henry Roticho kuwalaumu maafisa katika wiza ya Elimu haifai kwani majukumu ya wizara hizi mbili yanategemeana na yanafaa kutekelezwa kwa ushirikiano.