Makala

TAHARIRI: Harambee yahitaji malezi ya hadhi kuu

June 29th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

HUKU fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zikiendelea kushika kasi, mambo kadhaa yamejitokeza yanayohitaji serikali na viongozi wa kandanda nchini wayasahihishe punde kabla ya mashindano mengine makubwa kufanyika.

Unapouangalia mchezo wa Kenya na hata Tanzania, unagundua kuwa timu hizi mbili za kandanda hazina mchezo wa kiwango cha kimataifa.

Hii yakini ndiyo maana zilipokutana na Algeria na Senegal zilishindwa kutamba kabisa kiasi kwamba timu hizi hazikuweza kulenga hata shuti moja langoni pa wapinzani kwenye mechi zao za ufunguzi.

Naam, Algeria na Senegal ni timu za hadhi ya juu barani Afrika, lakini hazifai kulemea timu za ukanda huu jinsi zilivyofanya kwenye mechi hizo za mwanzo.

Harambee Stars, kutokana na mchezo duni, ilifungwa na Algeria 2-0 huku Taifa Stars ya Tanzania ikifumwa pia 2-0.

Swali linakuwa je, ni nini ambacho Harambee Stars inahitaji kufanya ndipo iweze kutatizana na timu pinzani za hadhi katika midani ya kimataifa?

Kwa uchanganuzi wa ndani, wachezaji wa timu kama Algeria wanaonekana kuwa na maarifa ya ziada uwanjani mbali na kwamba wana sifa zote nyingine zinazomilikiwa na timu nyingine za kawaida; kuwa thabiti kimwili na mbinu za kucheza mpira.

Ili kufaulu katika hili, ni muhimu serikali iwekeze zaidi katika vipawa. Itakuwa muhimu vituo vya mafunzo ya michezo kama vile soka na raga vibuniwe ili vijana wenye vipawa waweze kupewa utaalamu zaidi.

Mchezaji anapokuwa uwanjani mbali na kuhitajika kumiliki mbinu za kipekee za uchezaji, anafaa awe mpevu anayetumia ubongo wake kwa kasi ndipo aweze kutambisha timu katika kandanda ya leo.

Hivyo ndivyo timu zilizobobea zinavyofanya.

Yamkini mtaala mpya wa elimu (CBC) unaozinduliwa kwa sasa unaweza kusaidia kutimiza hili kwani mwanafunzi mwenye talanta atatambuliwa mapema na kuanza kupewa malezi yanayostahili afikapo kidato cha pili.

Hata hivyo, serikali haifa kusubiri hadi matokeo ya mfumo huo wa elimu yakweze hadhi ya Kenya michezoni, maadamu yatakuja baada ya muda mrefu.

Badala yake inahitajika kubuni vituo kadhaa vitakavyoanza kukuza talanta upesi.

Miundomsingi pia inahitajika. Pawepo na viwanja vya kutosha vyenye hadhi ili vijana wavitumie kukuza talanta zao. Hili pia liandamane na ufadhili wa michezo.