Makala

TAHARIRI: Hatua ya kufunga shule duni inafaa

September 27th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

HATUA ya serikali ya kufunga shule zisizotimiza kanuni zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kuwa na majengo salama inafaa.

Hatua hiyo ilijiri baada ya maafa kutokea katika shule ya Precious Talent Academy mtaani Kawangware ambapo wanafunzi wanane walipoteza maisha yao na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.

Kufikia jana, serikali ilikuwa imefunga shule nne za kibinafsi ikiwa ni pamoja na kufutilia mbali leseni ya shule ya Precious Talent Academy.

Ni wazi kuwa kama maafa hayo yasingetokea, shule ambazo zimefungwa katika mitaa ya Kibera na Kangemi zingekuwa zinaendelea kuhudumu pengine hadi mkasa utokee.

Hata inapokagua shule zote za kibinafsi nchini, serikali haiwezi kuepuka lawama ikizingatiwa kuwa ina idara inayohusika na kutathmini viwango vya ubora katika shule na masomo kwa jumla. Tunavyofahamu ni kuwa, maafisa wa idara hiyo wanafaa kuwa wakitembelea shule mara kwa mara kuhakikisha zinatimiza mahitaji yote ya ubora na usalama.

Kama idara hiyo ingetekeleza majukumu yake ipasavyo, mkasa uliosababisha maafa ya wanafunzi wanane wasio na hatia usingetokea. Hivyo basi, hatua zinapochukuliwa wamiliki wa shule wanaokiuka sheria, maafisa husika katika wizara wanafaa kuchukuliwa hatua pia.

Aidha, ukaguzi huo haufai kuwa shughuli ya uhusiano mwema ili kufumba watu macho baada ya mkasa wa majuzi. Unafaa kudumishwa kila wakati, si tu katika shule za kibinafsi bali pia za umma.

Tunasema hayo kwa sababu kuna shule za umma ambazo ziko katika hali mbaya sana kuliko za kibinafsi ambazo serikali imeanza kufunga.

Ikizingatiwa kuwa wazazi walikuwa wamelipa karo katika shule zinazofungwa, serikali inapaswa kuhakikisha wanafunzi hawakatizi masomo yao kwa kuwahamishia shule za umma zilizo karibu. Itakuwa dhuluma kwa watoto hao wakinyimwa haki yao ya kupata elimu.

Kumekuwa na madai kwamba baadhi ya walimu wakuu wa shule za umma wamekuwa kizingiti kwa wazazi wakitaka kuhamishia huko watoto wao huku wakiwaitisha ada kubwa kupindukia.

Kumekuwa na maswali kuhusu kiwango cha ubora wa masomo katika shule za umma kwa sababu ya uhaba wa walimu na vifaa. Hizi, pamoja na uhaba wa shule za umma, ni baadhi ya sababu zinazofanya shule za kibinafsi kuchipuka hasa katika mitaa ya mijini. Wanafunzi watendewe haki.