Makala

TAHARIRI: Hongera kudhibiti visa vya wizi KCPE

November 21st, 2018 2 min read

NA MHARIRI

Maafisa wa Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini (Knec), Wizara ya Elimu na wenzao wa Usalama wa Ndani wanastahili pongezi kwa jitihada zao kuhakikisha visa vya wizi wa mitihani ya kitaifa vimepungua maradufu.

Kama alivyotangaza waziri wa Elimu Amina Mohamed, huenda huu ukawa ndio mtihani wenye visa vichache zaidi vya wizi katika historia ya mtihani huo.

Na jambo la kufurahisha ni kwamba, watahiniwa wa mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) wamedhihirisha kwamba, bado watoto wetu wanaweza kufanya vyema bila kushiriki katika uozo huo wa kuiba mtihani.

Ingawa Serikali imetangaza kwamba watahiniwa wote zaidi ya milioni moja waliofanya mtihani wao mwaka huu watapata fursa ya kuendelea na elimu ya juu baada ya zoezi la kuteua wale watakaojiunga na shule za upili baadaye mwezi ujao, bila shaka tunatilia shaka ahadi hiyo.

Ili watahiniwa wote wapate fursa ya kusonga mbele na masomo yao, wizara hiyo haina budi kuweka mikakati kabambe kuhakikisha shule zilizopo zimepanuliwa na vile vile vyuo vya kiufundi vimeongezeka ili kukidhi mahitaji ya wale ambao bila shaka hawatapata fursa ya kuendelea na masomo yao.

Kila mwaka, shule zote za upili nchini huteua sehemu tu ya watahiniwa wa mtihani huo wa KCPE. Hatujui ni muujiza gani utatendeka wakati huu ili shule chache zilizopo ziweze kuwateua watahiniwa wote kwa wakati mmoja.

Vile vile, huku wanafunzi, wazazi na walimu wakiendelea kusherehekea matokeo bora ya mwaka huu, kuna suala la mimba za mapema ambalo limetishia kuwa janga la kitaifa endapo halitashughulikiwa kwa wakati unaofaa.

Kinyume na miaka iliyopita, idadi kubwa ya wanafunzi walipachikwa mimba na wengi wao ama wakalazimika kufanya mitihani hiyo muda mfupi baada ya kujifungua au wengine kuacha mtihani huo kabisa. Jambo la kukeketa maini ni kwamba, wahusika wakuu kwenye uhalifu huo ni walimu ambao wanapasa kuwa walezi wa watoto hao.

Tunahimiza waziri Amina kwa ushirikiano na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kufanya kila wawezalo kuhakikisha wahalifu hao waliojigubika kwa ngozi ya walezi wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ni matumaini yetu kwamba, ufanisi ulioshuhudiwa katika KCPE utapatikana tena katika mtihani unaoendelea wa Kidato cha Nne (KCSE) ili hadhi ya vyeti vya Kenya idumishwe kwa mara nyingine.