Makala

TAHARIRI: Huduma Namba ina manufaa tele

April 2nd, 2019 2 min read

NA MHARIRI

Ikiwa mpango wa matumizi ya mpya ya usajili na utambuaji wa Wakenya utafanikiwa, basi wananchi watakuwa na mengi ya kufaidika nayo kutokana nayo.

Katika hotuba ya Uhuru Kenyatta alipokuwa akizindua matumizi ya Huduma Namba katika eneo la Masii, Kaunti ya Machakos, rais alifichukua kwamba tayari takribani maafisa wa polisi hewa 5000.?wamegunduliwa wakipokea mishahara kwa njia ya udanganyifu.

Rais Uhuru alieleza kuwa kupitia mpango, kwa muda wa mwaka mmoja serikali ingeokoa Sh1.8b katika idara ya polisi pekee. Ikiwa kiasi hiki kikubwa cha fedha kingeokolewa kwa sekta hii pekee, je, ni kiasi gani kitaokolewa katika sekta zingine?

Bila shaka ikiwa mpango huu utakumbatiwa na wadau wote, Kenya itapata faida kubwa. Bali na kuokoa pesa, wananchi wataokoa wakati kwani kupata huduma itakuwa rahisi kwa kuwa habari zote zinazomhusu anayehudumiwa zitakuwa tayari kwenye namba hiyo na hivyo hakutakuwa na haja ya mahojiano mengi.

Kwa njia hii, basi itakuwa jambo la kufadhaisha kuona baadhi ya raia na viongozi kupinga mradi huu kwa kuendesha uvumi usio na mashiko wala maantiki yoyote. Si vyema kudai kwamba namba hii ni ya ‘kishetani’ na ina nia ya kumulika wanaume walio na mipango ya kando na watoto waliozaa nje ya ndoa! Kamwe huu si ukweli.

Manufaa zaidi kutokana na namba hii ni kwamba, itaweza kusaidia kukabiliana na ugaidi kwa sababu habari kuhusu kila Mkenya itakuwa ikipatikana kwenye habari ya historia ya mmiliki wake.

Aidha idadi ya watoto shuleni itakuwa ikijulikana moja kwa moja na hivyo basi kusaidia ukadiriaji wa utoaji hela za kuwasomesha bila tashwishi.

Fauka hayo, usajili huu utaweza kufichua washiriki wa ufisadi ambao Rais tayari ametangaza kuupiga vita vikali akishirikiana na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ili kutimiza malengo ya Ajenda Nnne Kuu za maendeleo.

Hata hivyo, itakuwa vibaya mno ikiwa mpango huu utaanza kwa kasi kisha usambaratike kabla manufaa yake kuonekana na wananchi.

Vivyo hivyo, itakuwa jambo lisilofaa ikigunduliwa kwamba kuna maana fiche hasa ya kisiasa na kwamba inalenga watu fulani.

Itakuwa jambo la kuridhisha ikiwa mpango huu utatekelezwa kwa njia ya kuaminiana, haki na ukweli ili lengo lake litimizwe kama inavyokusudiwa. Bila shaka Wakenya wote wafaa kuunga mkono mia kwa mia.