TAHARIRI: Ibainishwe mbona chanjo inakataliwa

TAHARIRI: Ibainishwe mbona chanjo inakataliwa

KITENGO CHA UHARIRI

SERIKALI imekuwa ikishinikiza wananchi kuendea chanjo ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona kwa muda mrefu sasa.

Chanjo zilianza kuletwa kwa viwango vidogo awali, na ni watu wachache ambao walikuwa wanaruhusiwa kuzipokea.

Walijumuisha makundi ya watu ambao wako hatarini kuambukizwa ama walio hatarini kuathirika zaidi kiafya endapo wataambukizwa virusi hivyo.

Makundi hayo yalijumuisha watu kama vile wahudumu wa afya, walimu, maafisa wa usalama na wazee.

Hata hivyo, takwimu zilizopo kutoka kwa Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa wengi hawajaendea chanjo hizo licha ya kuwa walipewa kipaumbele.

Miongoni mwa wale ambao walijitokeza kwa awamu ya kwanza, wengi wamekataa kuendea ya pili jinsi inavyohitajika kwa madhumuhi ya kupata kinga kamili.

Jumanne, iliibuka kuwa serikali sasa inataka watumishi wote wa umma waende kupokea chanjo ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

Katika baadhi ya mataifa, kuna mashirika ambayo tayari yameanza kuwasimamisha kazi au kuzuia wafanyakazi kuingia afisini iwapo hawajapokea chanjo dhidi ya Covid-19.

Sababu za watu kukataa kupokea chanjo hizo ni tofauti, lakini kuna uwezekano wengi wanazisusia kwa sababu pengine hawajaamini hatari ya Covid-19 kwa maisha ya mamilioni ya binadamu au hawajapokea habari za kutosha kuhusu usalama wa chanjo zinazoendelea kuagizwa kutoka nchi za kigeni.

Katika enzi hizi ambapo habari husambaa kwa kasi, inasikitisha kuwa habari za kupotosha hufikia watu wengi hata kuliko zile za kweli.

Ni wajibu wa asasi za serikali zinazosimamia masuala ya afya kutia bidii katika usambazaji wa habari sahihi na kwa njia inayoaminika kuhusu chanjo za kuepusha corona.

Kabla tufikie hali ambapo serikali huenda ikaamua kuanza kutumia vitisho dhidi ya umma ili waende kupokea chanjo kwa lazima, ni muhimu kuwe na juhudi za kusambaza maelezo yote, ikiwemo athari zozote kama zipo kuhusu chanjo.

Janga la corona limetufunza kuwa, vitisho pekee havitoshi kushawishi watu kubadili tabia zao.

Hii ni wazi kutokana na jinsi, licha ya raia kuonyeshwa wagonjwa mahututi na makaburi ya jamaa waliokufa kwa Covid-19, idadi kubwa mno bado hawajali kufuata kanuni za kujilinda dhidi ya maambukizi.

You can share this post!

NGILA: Toka mjini, uchumi wa kidijitali umefika vijijini

Afueni ya muda kwa Zuma, korti ikiahirisha kesi