Makala

TAHARIRI: Idara ya mahakama itengewe pesa zaidi

November 6th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

MOJAWAPO ya vigezo vinavyotumika na nchi zilizostaaratibika kuamua iwapo zitawekeza katika taifa fulani au la ni hali ya mfumo wa sheria wa nchi hiyo na iwapo utawala wa sheria unakumbatiwa.

Hatua ya Kiongozi wa Idara ya Mahakama nchini Jaji Mkuu David Maraga kujitokeza hadharani na kuelezea masaibu yake na idara hiyo kwa jumla mikononi mwa serikali kuu inapasa kuwatia wasiwasi wote wanaopigania mfumo wa utawala wa sheria ambapo maamuzi yote yanaelekezwa kwa misingi ya usawa na haki.

Katika siku za hivi majuzi, majaji na mahakimu nchini wamefanya maamuzi ambayo yanakinzana na matakwa ya serikali kuu.

Maafisa wakuu serikalini wamelalamikia kile wanadai kuwa ni hujuma kutoka kwa wakuu wa mahakama ambapo kesi zinacheleweshwa na wahalifu kuachiliwa kwa masharti nafuu.

Baadhi ya malalamishi hayo huenda yana mashiko ikizingatiwa kwamba, hakuna washukiwa wanaotekeleza uhalifu wa kiuchumi wamewahi kushtakiwa na kutupwa jela kwa makosa yao.

Lakini hilo si sababu tosha ya serikali kuu kudhalilisha mahakama kama hali ilivyo kwa sasa.

Idara ya Mahakama ni mojawapo ya matanzu matatu makuu ya serikali. Mengine ni Serikali Kuu na Bunge. Kwa mujibu wa Katiba, nguzo hizo tatu kuu ziko huru. Kila moja inapasa kujitegemea.

Lakini hali iliyopo ambapo bajeti ya mahakama imepunguzwa pakubwa kwa misingi ya kisiasa haifai.

Bunge linapasa kutathmini upya mapendekezo kuhusu kupunguzwa kwa bajeti hiyo ili shughuli za kawaida ziendelee katika mahakama zetu.

Jaji Mkuu aliangazia masuala mengi ambayo anahisi yanakwamisha utendakazi wa idara hiyo muhimu.

Hata hivyo, wakosoaji wa idara hiyo wanasema majaji hawawajibikii yeyote na pia hawasaidii serikali kwenye kampeni ya kupambana na ufisadi. Huenda yote hayo ni kweli, lakini kulemaza idara nzima ya mahakama kwa kuinyima mgao wake wa bajeti haifai.

Ni matumaini yetu kwamba, wakuu wa matapo hayo matatu ya serikali watatafuta mbinu ya kushirikiana kwa manufaa ya Wakenya.

Tungependa kuamini kwamba, hatua za serikali hazitokani na onyo la Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2017 alipochemka na kuonya Mahakama kwamba, angechukua hatua ‘zifaazo’ dhidi ya majaji baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha ushindi wake.

Kwa kufanya hivyo ni kushusha hadhi ya idara hiyo muhimu ambayo ni mhimili wa usawa na haki kwa mwananchi wa kawaida.