TAHARIRI: IEBC ihakikishe wanasiasa wanaoshiriki harambee wanaadhibiwa

TAHARIRI: IEBC ihakikishe wanasiasa wanaoshiriki harambee wanaadhibiwa

KITENGO cha UHARIRI

KUANZIA leo, ni marufuku kwa wanasiasa wanaopania kuwania nyadhifa mbalimbali kushiriki katika hafla za kuchangisha fedha, maarufu kama harambee.

Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapiga marufuku wanasiasa kushiriki katika hafla za kuchangisha fedha miezi minane kabla ya uchaguzi mkuu.Lengo la sheria hiyo ni kuzuia wanasiasa kutumia fedha kuwashawishi wapigakura kuwachagua.

Tume ya IEBC tayari imeonya kuwa wanasiasa watakaokiuka marufuku hiyo wataadhibiwa, ikiwemo kuzuiliwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.Onyo hilo la IEBC lisiwe vitisho baridi – bali wanasiasa watakaoshiriki katika michango hiyo waadhibiwe bila kujali vyeo au wingi wa wafuasi wao.

Kila uchaguzi, IEBC imekuwa ikitoa vitisho bila kuchukua hatua hivyo imefanya wanasiasa kuichukulia kama asasi isiyong’ata.Wakati wa uchaguzi, wanasiasa wamekuwa wakinaswa wakisambaza fedha kwenye foleni ambapo watu wanangojea zamu yao kupiga kura.

Tumeshuhudia wanasiasa wakitundika mabango makubwa ya kujipigia debe hata kabla ya IEBC kutangaza rasmi kuanza kwa kampeni.Jana, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, alilalamikia kampeni za mapema ambazo zimekuwa zikiendeshwa na wanasiasa mbalimbali, wakiwemo Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, ni haramu.

Kwenye taarifa aliyotoa jana baada ya mkutano kati ya tume hiyo na Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) mjini Limuru, Kaunti ya Kiambu, Bw Chebukati alisema kuwa kampeni za mapema ni hatia kwa mujibu wa Sheria ya Uhalifu wa Uchaguzi ya 2016.

Bw Chebukati alisema kwamba Kifungu cha 14 cha Sheria ya Uchaguzi kimepiga marufuku kampeni za mapema na hata kutundika mabango ya kujipigia debe.Kifungu cha 13 cha Sheria ya Uhalifu wa Uchaguzi, kinasema kuwa mwanasiasa anayekiuka marufuku hiyo atozwe faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitano gerezani au adhabu zote mbili.

Lakini wanasiasa wamekuwa wakikiuka bila kuadhibiwa. Hii inatokana na ukweli kwamba IEBC inakumbwa na uhaba wa maafisa wa kuhakikisha kuwa sheria hiyo inatekelezwa kikamilifu na wanasiasa.Kuna uwezekano kwa wanasiasa kutumia mwanya huo kushiriki michango kinyume cha sheria.

Watajifanya kutoa sadaka nono makanisani wakidai wanamtumikia Mungu. Pia watajifanya kufariji wafiwa kwa kutoa michango minono. Tume ya IEBC iwe macho kuwaadhibu wote.

You can share this post!

Masonko waelezea sababu kuunga Raila kidole

Uhuru ataacha deni la ahadi alizotoa kwenye kampeni- Ruto

T L