Makala

TAHARIRI: IEBC ijiandae kwa chaguzi ndogo

August 10th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inafaa sasa itoe mwelekeo kuhusu chaguzi ndogo ambazo zilikuwa zimeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Baada ya kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kutangazwa nchini, tume hiyo iliamua kuahirisha chaguzi ndogo katika wadi nne na eneobunge moja.

Wadi ambazo hadi sasa hazina diwani ni Kahawa Wendani iliyo Kaunti ya Kiambu, Dabaso katika Kaunti ya Kilifi, Kisumu Kaskazini katika Kaunti ya Kisumu, na Wundanyi Mbale katika Kaunti ya Taita Taveta.

Hali sawa na hii inakumba wakazi wa eneobunge zima la Msambweni, Kaunti ya Kilifi ambao mbunge wao alifariki. Inaeleweka kuwa IEBC haikuwa na budi ila kuahirisha chaguzi ndogo ya kuwapa wananchi wa maeneo hayo viongozi wapya.

Lakini sasa, shughuli nyingi za kwaida zimeanza kurudi nchini na bila shaka, kuna jinsi ambavyo tume hiyo inaweza kushirikiana na wataalamu wa afya kupata njia bora ya kufanikisha chaguzi hizo bila kuhatarisha maisha ya wananchi.

Maafisa mbalimbali wa tume hiyo akiwemo mwenyekiti wake, Bw Wafula Chebukati, wamewahi kunukuliwa wakisema kuna mashauriano yanaendelezwa kutafuta mwelekeo mwafaka kuhusu chaguzi hizo.

Hata hivyo, kufikia sasa, haijabainika wazi hatua zilizopigwa na wananchi wameanza kuwa na wasiwasi. Wakati huu taifa linalokumbwa na janga la corona lililotikisa ulimwengu mzima, wananchi wanahitaji uwakilishi karibu nao.

Hii ni kutokana na kuwa wanapitia hali ngumu na wanatakikana kupata mtu ambaye atawasilisha kilio chao kwa mamlaka husika kwa urahisi.

Tumeshuhudia katika maeneo mbalimbali jinsi wabunge na madiwani kadhaa wanavyohusika pakubwa kutetea masilahi ya raia ili wasisahaulike wakati serikali inapotoa misaada kwa wanaoathirika na janga la corona.

Kwa msingi huu, ni wazi kuwa wale wasio na wawakilishi wanatatizika sana na haki zao zinakandamizwa wasipokuwa na wawakilishi katika bunge la kaunti na kitaifa.

Vile vile, IEBC inaweza kutumia chaguzi hizo ndogo kuthibitisha uwezo wao wa kuandaa uchaguzi wowote ule wakati kunapokuwa na janga aina hii.

Hakuna anayejua janga la corona litakapotuondokea, kwa hivyo inafaa kila asasi ijifunze jinsi ya kufanikisha majukumu yao chini ya kanuni kali za kiafya zilizopo.