TAHARIRI: IEBC isikubali presha za mirengo, ifuate sheria

TAHARIRI: IEBC isikubali presha za mirengo, ifuate sheria

NA MHARIRI

MKUTANO wa jana Jumatano kati ya wagombeaji urais kwenye uchaguzi mkuu ujao na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ulianika misimamo tofauti kuhusu sajili ya kura na upeperushaji wa matokeo.

Kila upande uliwasilisha matakwa yake na kuyatetea mbele ya tume.

Japo ni jukumu la tume kuhakikisha mchakato wa kuandaa uchaguzi unashirikisha wadau wote katika kila awamu na hasa wagombeaji wa urais, ni muhimu kufahamu kuwa kila mrengo, huwa unatoa msimamo na matakwa ya kulinda maslahi yake.

Katika hali hii, wasimamizi wa tume wanaweza kujipata katika hali tata wakichukua hatua kupendeza mrengo mmoja.

Kwa mintaarifu hii basi, tume inafaa kuchukua msimamo usiotetereka mradi tu inazingatia sheria na katiba katika kutekeleza majukumu yake ya kuandaa uchaguzi huru, haki na wa kuaminika.

Hakuna wakati hata mmoja ambao wanasiasa wanaoshindana hasa katika uchaguzi wa urais watakubaliana katika masuala yote na kuwasikiliza kunaweza kuchosha.

Tume kama mwamuzi wa uchaguzi mkuu, inafaa kuchukua msimamo kwa kuzingatia sheria na ndani ya mamlaka yake, kufahamisha wagombeaji bila kusalimu amri kwa sababu ya presha za mirengo ya kisiasa.

Ikiwa tume inayosimamiwa na Bw Wafula Chebukati ilikita hatua ilizochukua katika uamuzi wa Mahakama ya Juu uliobatilisha matokeo ya kura ya urais mwaka wa 2017, na iliuafikia kwa kuzingatia sheria na katiba, kukubali matakwa yote ya wanasiasa kunaweza kuvuruga mipango yake.

Kwa kukita mchakato wake wa uchaguzi mkuu ujao katika uamuzi huo, tume inalenga kurekebisha makosa yaliyofanya matokeo ya kura ya urais kufutwa 2017.

Inafaa kukumbukwa kuwa ni wanasiasa waliopeleka kesi kortini na kupitia mawasilisho yao, majaji wakaamua kuwa uchaguzi wa urais haukuweza kuaminiwa kwa sababu ya mchakato uliotumiwa.

Hivyo basi, iwapo inahisi matakwa ya wagombeaji urais yanakinzana na uamuzi wa Mahakama ya Juu au yanaweza kutia ndoa mchakato wa uchaguzi mkuu ujao, na iwapo baada ya kutathamini, kuchaganua, kuhakiki na kushauriana kwa mapana kwamba hatua ilizochukua zitahakikisha mchakato na mifumo iliyoweka itahakikisha uchaguzi utakuwa wa kuaminiwa, haifai kuyumbishwa na misimamo ya mirengo ya kisiasa.

Hata hivyo, baada ya kuwasikiliza wagombeaji, inachopaswa kufanya ni kuziba mianya iliyotambua ili kutia nguvu mifumo yake.

Hivi ndivyo Bw Chebukati na tume yake inafaa kufanya hata inapoendelea kukamilisha maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao. Bila shaka ina kibarua na ni kwa kuzingatia sheria na katiba ambapo itafanikiwa.

  • Tags

You can share this post!

Kiraitu aapa kuangusha Mbunge uchaguzini ubabe kati yake na...

Moraa na Korir mawindoni Stockholm Diamond League kinyume...

T L