TAHARIRI: IEBC iweke kanuni nzuri za kuwachuja wasimamizi

TAHARIRI: IEBC iweke kanuni nzuri za kuwachuja wasimamizi

NA MHARIRI

WAKENYA wanapoendelea kusubiri matokeo ya uchaguzi wa urais, hapana budi kuishukuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Wafula Chebukati, ameonyesha ukomavu wa hali ya juu katika jinsi anavyoshughulikia matumaini ya wananchi.

Kwa kuelewa kwamba shughuli ya kuthibitisha matokeo ingechukua muda mrefu, alianza kwa kuuwekea wazi ulimwengu matokeo ya kura zilizohesabiwa vituoni.

Maafisa wake wanapong’ang’ana ili kuwa na matokeo kamili ya kura za urais, wameonyesha pia ukomavu na kufanya kazi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu.

Hata hivyo, baadhi ya dosari ambazo zimejitokeza wakati wa kuhesabu kura kwenye vituo vya maeneobunge zinaibua maswali kuhusu umakini wa IEBC wakati wa kuwasajili.

Wakati wa kujumlisha kura, kuna taarifa za maafisa wa usimamizi wa uchaguzi waliopatikana wakiwa wamebeba karatasi za kura zilizo na alama.

Katika kisa kimoja, msimamizi wa uchaguzi alifungia ndani ya sanduku la kura nyaraka muhimu pamoja na fomu 34A.

Kuna kisa pia cha msimamizi mwengine ambaye aliwakataza wanahabari kuingia kwenye ukumbi wa kujumlisha kura.

Aliwafukuza hata baadhi ya maajenti huku akiruhusu wanasiasa.

Mambo haya na mengine mengi ambayo yamefanya baadhi ya maafisa hao kufunguliwa mashtaka, yanafanya Wakenya washuku mfumo unaotumiwa kuajiri makarani.

Ni wazi kuwa shughuli ya kuwapiga msasa wasimamizi wa uchaguzi huharakishwa. IEBC ingehoji watu hao punde shughuli ya mchujo inapoanza, ili wapate uzoefu wakazi hiyo.Kinachohitajika zaidi ni kanuni bora za kuwatambua maafisa ambao huenda hawajakomaa kimaadili.

You can share this post!

Chebukati ataka polisi wachunguze aliko afisa

Chebukati ahimizwa akaze mkono ili kumaliza taharuki

T L