Makala

TAHARIRI: Jamii ikomeshe mimba za watoto

June 29th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

HISIA tofauti zilitolewa baada ya ripoti kuibuka kuhusu idadi kubwa ya watoto ambao wameshika mimba kitaifa tangu mwaka 2020 ulipoanza.

Kuna viongozi na wananchi ambao waliamua kupuuzilia mbali ripoti hizo, na wengine ambao walisisitiza zichukuliwe kwa uzito.

Ijapokuwa maswali mengi yaliibuka, kile kinachofaa kusisitizwa ni kwamba idadi ya wasichana wadogo wanaotungwa mimba yazidi kuongezeka.

Ni aibu tunaposikia kiongozi serikalini anapotoa matamshi yanayoonyesha kama kwamba jambo hilo ni la mzaha ilhali ana mamlaka ya kushinikiza sera na sheria ambazo zitasaidia watoto kuepuka kujiharibia maisha yao.

Wakati kiongozi anapolaumu mitandao ya kijamii na Intaneti kwa mimba za mapema zinazoongezeka, ni wazi kuwa hana haja kufanya uchunguzi na kufafanua hali halisi ilivyo.

Kuna wasichana wengi ambao wanaishi vijijini, kwa hali ya umasikini mkubwa wasioweza hata kugharamia chakula ilhali wengine wanataka tuamini wana uwezo wa kugharamia mitandao kujifunza usherati.

Wengine wengi hubakwa kwa nguvu na wazee, huku idadi nyingine kubwa wakihadaiwa kwa sababu ya umaskini wanaopitia katika familia zao, bila kusahau wanaolazimishwa kuingia katika ndoa za mapema.

Kuna pia wasichana ambao hushika mimba wanaposhiriki tendo la ndoa na wavulana wa rika zao.

Hatukatai kuwa uimarishaji wa Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) umechangia kwa kiwango fulani watoto kujifunza mambo ya kupotosha ikiwemo kuingilia ngono mapema.

Hata hivyo, ili kutatua kikamilifu janga hili linaloharibia mtoto wa kike maisha yake, ni muhimu suala hilo litazamwe kwa mapana.

Wadau wanafaa kutambua chanzo halisi cha janga hili. Ikiwa itaamuliwa kwamba mbinu bora zaidi ya kukabiliana na tatizo hilo ni kwa kudhibiti mitandao, tutakuwa katika hatari ya kufanya mambo kwa ubaguzi. Hii ni kutokana na kuwa, idadi kubwa ya wasichana hasa walio vijijini watakuwa wangali katika hatari ya kupata watoto wakiwa na umri mdogo.

Changamoto na mienendo ya kimaisha inayosukuma wasichana kujihusisha kwa ngono wakiwa wadogo zitambuliwe na kutatuliwa.

Viongozi wajitolee kikamilifu kuwekeza rasilimali za kutosha katika kutafuta mbinu ambazo zitaokoa wasichana.