Makala

TAHARIRI: Jamii yafaa ijitolee kuzima ‘usponsa’

January 27th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

KWA muda mrefu sasa, suala la ‘usponsa’ limekuwepo katika jamii yetu. Idadi kubwa ya wasichana wanaotekwa katika mipangilio hii ya kuwanufaisha wanaume wazee sana kuliko ‘mawindo’ yao ambayo ni wanafunzi wa vyuo vikuu.

Wanaume wanaoingilia maelewano hayo huwafaidi wasichana hao kifedha na kwa mahitaji mengine mengi.

Inafahamika kwamba idadi kubwa ya wanaume hao huwa wameoa, mbali na kuwapo uwezekano kuwa wana wapenzi wengine wengi wa pembeni.

Si siri, kuna wanafunzi wengi vyuoni ambao hupitia maisha magumu na huenda hili ndilo huwasukuma kukubali ‘kuuza’ miili yao kwa wanaume bila kujali hatari wanayojiweka ndani yake maishani.

Licha ya hayo, wasichana wengine husukumwa na tamaa ya maisha ya kifahari, mbali na shinikizo kutoka kwa wenzao ambao pengine hutoka katika familia za kitajiri zinazoweza kugharimia chochote wanachotaka mabinti zao.

Jamii inastahili kujitokeza kwa ukakamavu zaidi kukemea suala hili la usponsa kwani halina tofauti na ukahaba.

Cha kusikitisha zaidi ni jinsi wanaolengwa ni wasomi ambao ndio tegemeo la kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi hii katika miaka ijayo.

Ijapokuwa ujana ni moshi, kuna makovu ambayo yatasalia katika jamii kwa miaka ijayo iwapo tutaendelea kufumbia macho tabia hii inayopotosha maadili ya kidini na ya kijamii, kwa wale watakaodai si waumini wa dini yoyote.

Hatuwezi kulaumu wasichana pekee, bali pia waume ambao huacha familia zao nyumbani kwenda kujiburudisha na wasichana hao wadogo wanaoweza kuwa hata mabinti wao.

Shida iliyopo si uozo wa maadili ya kijamii pekee bali pia hatari ya kueneza magonjwa ya zinaa. Wakati mwanamume anapoviziavizia msichana mdogo katika chuo kikuu, bila shaka kuna uwezekano mkubwa ana wengi wa pembeni kando na mke wake wa ndoa.

Inafaa jamii ijihoji kuhusu tabia hizi na kutafuta mbinu zinazoweza kutumiwa kurudisha maadili mema miongoni mwa wananchi.

Tamaa ya kutafuta utajiri wa haraka na maisha ya kifahari miongoni mwa vijana isiachwe iharibu hatima yao ya siku za usoni, kwani hawa ni vijana wanaohitaji kupewa mwelekeo bora wa kimaisha wasije wakajutia baadaye.