Makala

TAHARIRI: Kampeni za 2022 hazimfaidi yeyote

August 23rd, 2018 2 min read

NA MHARIRI

Ni jambo la kusitikisha na vile vile kushangaza kwamba, mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, viongozi mbalimbali wa kisiasa wamezindua kampeni wakilenga viti tofauti katika uchaguzi wa 2022.

Huku kwa kweli ni kudunisha na kudhalilisha raia wa nchi hii waliomiminika katika vituo vya kupigia kura na kuwachagua viongozi hao mwaka uliopita.

Viongozi hao walitoa msururu wa ahadi wakati wa kampeni za uchaguzi. Waliahidi kujenga barabara mpya, kusambaza maji safi vijijini, kusambaza nguvu za umeme katika kila pembe ya nchi na muhimu zaidi, kuhakikisha raia wa nchi hii wanapokea matibabu kwa gharama ya chini.

Ingawa tumo kwenye viwango tofauti vya ufanisi katika utekelezaji wa miradi hiyo, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinapasa kuondolewa ili Wakenya wafurahie maisha kama wenzao kwingineko duniani.

Kampeni za kisiasa kwa kawaida huibua msisimko na hupandisha joto la kisiasa. Migawanyiko mikubwa hutokea huku majirani wakitofautiana kwa misingi ya misimamo yao ya kisiasa. Mbona viongozi wetu wakamie kuvuruga utulivu tunaofurahia baada ya kipindi kirefu cha kampeni mwaka jana?

Ni ubinafsi mkubwa kwa viongozi wanaoshikilia dau la nchi hii kuanza kampeni kwa zoezi litakalofanyika miaka minne ijayo bila kuwahudumia wananchi kwa sasa.

Isitoshe, baadhi ya viongozi kwa ujeuri mkubwa wanadai kulipwa madeni ya kisiasa miaka minne kabla ya uchaguzi mwingine kuandaliwa. Kwanza, tungependa kutaja hapa kwamba, hakuna deni katika siasa.

Wanasiasa wetu kama ilivyo kwingineko, huunda miungano ya kisiasa kwa lengo la kutwaa mamlaka. Hivyo basi, ni kinaya kwamba wale wanaodai madeni fulani ya kisiasa ndio wamo usukani mwa ngalawa kwa sasa. Ni tamaa iliyoje kwa kiongozi kupuuza vinono vilivyoandaliwa mezani na kuanza kudondokwa na mate kwa kuwazia vilivyo umbali wa miaka minne?

Ombi letu kwa wanasiasa ni kutumia nguvu, uwezo wao na raslimali zilizopo kuhakikisha wanaboresha hali ya maisha ya raia wa Kenya ambao wengi wao hawana namna ya kujipatia mkate wao wa kila siku.

Ni kudunisha raia wenzao kwa wanasiasa hao kuzunguka katika kila pembe ya nchi kujipigia debe kuhusu ufanisi tuliopata kama nchi ilhali kuna ushahidi tosha wa familia nyingi zinazoshinda mchana kutwa bila kutia chochote kinywani.

Wapiga kura wa sasa wana ufahamu mkubwa wa kisiasa na tunaamini wakati mwafaka ukifika, watawaadhibu kwa kuwatema wanasiasa kama hao ambao wanawatumia kama ngazi kujikweza kwa manufaa yao binafsi.