Makala

TAHARIRI: Kanuni za corona zizidi kufuatwa

June 8th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

WAKAZI wa maeneo ambayo yalifunguliwa na serikali baada ya kufungwa kwa wiki kadhaa, wanafaa kuendelea kufuata kanuni zote za kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

Jumapili, ilibainika wakazi hao wa Kaunti za Kwale na Kilifi na mitaa ya Old Town (Mombasa) na Eastleigh (Nairobi) walianza kurejelea shughuli zao za kawaida.

Inaeleweka kuwa wengi wao walitatizika sana kwa kipindi chote ambapo hawangeweza kuondoka maeneo hayo kihalali.

Vile vile, wale wanaofanya kazi na biashara zao katika maeneo hayo waliathirika sana kwani wateja wengi hawangeruhusiwa kuingia.

Kwa msingi huu, kuna uwezekano baadhi yao kusahau kuhusu umuhimu wa kuendelea kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona kwa vile wameeka akili zao katika kujaza hasara walizopata kwa muda huo wote.

Ni muhimu kila mkazi akumbuke chanzo cha kuwafanya kufungiwa na serikali, ambacho ni kuwa, maambukizi yalikuwa yanaongezeka kwa kasi.

Uamuzi wa kufungua ulitokana na kuwa maambukizi yalipungua kwa kiasi kikubwa katika maeneo hayo.

Si siri kwamba serikali haitasita kufunga tena eneo lolote ambapo idadi ya wagonjwa wanaougua Covid-19 itaongezeka kwa kiwango kikubwa.

Njia pekee ya kuzuia hatua hii kuchukuliwa, hasa kwa wale ambao sasa wako huru baada ya kufungiwa kwa muda, itakuwa ni kufuata kanuni zote za wataalamu wa afya kuhusu mbinu za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Kuna habari nyingi zinazoenezwa kila mahali kujaribu kudunisha hatari za virusi vya corona lakini itakuwa busara kufuata kile kinachoweza kuthibitishwa kufikia sasa.

Thibitisho lililopo ni kuwa, ugonjwa huo unaweza kusambazwa kwa kasi sana ikiwa watu hawafuati kanuni za wataalamu wa afya na pia unaweza kusababisha vifo vingi.

Wito wa kuendelea kujikinga usiwe tu kwa maeneo hayo yaliyofunguliwa bali kwa kila pembe ya taifa hasa kufutia kulegezwa kwa saa za kafyu.

Hakutakuwa na haja eneo moja kuweka mikakati thabiti ya kuepusha ueneaji wa virusi vya corona, ilhali maeneo mengine yamezembea.

Matokeo yake itakuwa kwamba ugonjwa huo utaingizwa kutoka eneo moja hadi lingine, na kurudisha nyuma hatua zilizopigwa katika vita hivi.

Ni wazi kuwa uwezekano wa nchi kurejelea hali yake ya kawaida ni kupitia kwa hatua zinazochukuliwa na kila mwananchi, kwa hivyo kuwe na ushirikiano kikamilifu.