NA MHARIRI
KENYA kwa mara nyingine imeingia katika kipindi kinachotarajiwa kusheheni visa vya mahangaiko ya wananchi wanaokumbwa na njaa.
Kwa mwaka wa tano mfululizo sasa, inatarajiwa kuwa maeneo ambayo kwa kawaida hupokea kiasi kidogo cha mvua yatakuwa makavu.Maeneo hayo yanapatikana humu nchini na pia katika mataifa mengine ya ukanda wa pembe ya Afrika.
Katika nchi hii, imekadiriwa kuna takriban wananchi milioni nne ambao wataathirika na njaa, kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa.
Inasikitisha kuwa, hili ni suala ambalo limekuwa likitokea tangu jadi ila hatujaona kukiwa na mipango ya kutosha kurekebisha hali.
Wakati serikali za ugatuzi zilipoanzishwa, kulikuwa na matumaini tele kwamba changamoto hii ingekuwa miongoni mwa zile ambazo zingezikwa kwa kaburi la sahau haraka iwezekanavyo hasa na magavana wa kaunti zinazokumbwa na kiangazi mara kwa mara.
Miaka kumi baadaye, hakuna chochote cha kuridhisha. Magavana wa kaunti husika wamebaki mstari wa mbele kufuata mbinu zile zile za jadi za kusubiri kuomba misaada kila wakati hali inapokuwa mbaya.
Wakati huu ambapo kiangazi kali inaendelea huku serikali mpya za kaunti zikiingia mamlakani, inasubiriwa kuonekana kama kuna kaunti yoyote itakayojitolea kutatua changamoto aina hii.
Baadhi ya magavana tayari washaonekana kufa moyo, wakitoa sababu kama vile uhaba wa fedha kuwa changamoto kwa mipango ambayo huenda walikuwa nayo kuboresha hali ya maisha kwa wananchi.
Ikiwa serikali za kaunti zinakumbwa na uhaba wa fedha, jambo la busara litakuwa ni kuangalia shughuli zisizo muhimu ili ziwekwe kando na fedha zitumiwe kufadhili miradi ambayo ina manufaa kwa wananchi.
Hatungependa kuona mabilioni ya pesa zikitumiwa kwa mambo yanayonufaisha watu wachache walio wandani wa magavana wakati ambapo mamilioni ya wananchi wanateseka kwa makali ya njaa.
Kwa upande wake, serikali ya kitaifa pia itimize wajibu wake kwa kukabidhi kikamilifu serikali za kaunti mamlaka ya kusimamia huduma zilizopeanwa kwa tawala za ugatuzi Kikatiba.
Baadhi ya sekta muhimu ambazo zinafaa kuwa chini ya serikali za kaunti bado zinadhibitiwa sana na serikali ya kitaifa kwa kiwango cha kuwa, serikali za kaunti zinakosa rasilimali za kutosha kuhudumia wananchi.
Serikali ya kitaifa inafaa tu kuwa mshirika wa zile za kaunti katika masuala ambayo Katiba ilikabidhi tawala za kaunti.
9*Kulikuwa na sababu mwafaka ya kugawa mamlaka wakati Katiba iliporekebishwa 2010 na hivyo basi hili ni jambo ambalo linafaa litekelezwe kikamilifu kwa maslahi ya wananchi.