TAHARIRI: Kaunti ziungane kwa maendeleo

TAHARIRI: Kaunti ziungane kwa maendeleo

KITENGO CHA UHARIRI

UAMUZI wa madiwani wa Kaunti ya Kilifi wiki iliyopita kupitisha hoja ya kutaka ushuru wa miraa na muguka uongezwe, uliibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi.

Madiwani walisema kuwa hatua hiyo ililenga kupunguza matumizi ya bidhaa hizo, ingawa pia itachangia kuongeza mapato ya serikali ya kaunti.

Mojawapo ya masuala yaliyoibuka baada ya uamuzi huo ni kwamba hoja hiyo ikiidhinishwa kuwa sheria ya kaunti, huenda ikawa vigumu kuafikia malengo yake hata ikitekelezwa kikamilifu.

Hii ni kutokana na kuwa Kaunti ya Kilifi imepakana na kaunti nyingine za Pwani ambako ni rahisi wakazi kuvuka wanapotaka, waende kununua bidhaa wanazotaka bila vikwazo vingi.

Hiyo inamaanisha kuwa iwapo hakutakuwa na vikwazo vingine kando na kupandisha ushuru wa bidhaa hizo, baadhi ya watumiaji watakuwa wakizitafuta katika kaunti jirani.

Swala hili limeibua mdahalo kuhusu hitaji la kaunti zinazopakana kushirikiana kuhusu sheria ambazo madiwani huwa wanabuni katika mabunge ya kaunti.

Baada ya utawala wa ugatuzi kuanza kutekelezwa mwaka wa 2013, magavana walianzisha mfumo wa kuunda miungano ya kaunti ambazo ziko katika kanda.

Kwa mfano, kaunti sita za Pwani ziliunda Jumuiya ya Kaunti za Pwani huku zile za Nyanza na Magharibi zikiunda Jumuiya ya Kaunti za Ukanda wa Ziwa Victoria.

Miungano hii kwa muda mrefu zilijikita katika mijadala kuhusu ushirikiano wa kiuchumi ingawa hakuna hatua kubwa ambazo zimeonekana mbele za umma kuhusiana na juhudi hizo zao.

Iwapo kaunti zitaendelea kujitenga katika sheria wanazobuni, kuna uwezekano hali hiyo italeta hasara kuliko faida zinazokusudiwa.

Kuna matukio mengi ambayo yamedhihirisha kuhusu umuhimu wa serikali za kaunti zinazopakana kushirikiana.

Tangu mwaka uliopita, janga la virusi vya corona lilituonyesha jinsi kaunti mbalimbali zilivyotegemeana katika utoaji wa huduma za matibabu.

Ushirikiano uliokuwepo na ambao bado upo miongoni mwa baadhi ya kaunti, ulifanywa bila mwongozo wowote mahususi.

Tunaamini kuwa iwapo kuna maelewano rasmi kati ya kaunti kuhusu jinsi zinavyoweza kushirikiana katika sekta mbalimbali muhimu kama vile afya, kilimo, maji, uchukuzi miongoni mwa nyingine, taifa hili litapata nafasi bora zaidi ya kufaidika kutokana na ugatuzi.

You can share this post!

Matamanio ya Ruto, uamuzi wa June na mja kupata ajaliwalo...

WANGARI: Ukiritimba ukomeshwe Kenya Power ili kuboresha...