Maoni

TAHARIRI: Kenya haiwezi kujistawisha kwa ushuru huu uliopitiliza

May 20th, 2024 2 min read

WATAALAMU wa masuala ya uchumi wamekariri mara si moja kuwa hakuna taifa lolote duniani lililopiga hatua kiuchumi kwa kuzidisha ushuru.

Wengi wanaifananisha hali hiyo na mtu aliyekalia beseni anayejaribu kujinyanyua. Haiwezekani.

Mswada wa Fedha wa 2024 utakaopitishwa bungeni, bila kizuizi, umebeba aina mpya za ushuru wa kushangaza.

Hii ni mbali na ushuru ulioasisiwa au kuongezwa na Sheria ya Fedha ya 2023 kama vile Ushuru wa Nyumba, nyongeza ya ushuru wa VAT kwenye bidhaa za mafuta kutoka asilimia nane hadi 16, Ushuru wa Mapato ya Jumla kwa biashara ndogondogo na kadhalika.

Mswada unaotazamiwa kupitishwa bungeni hivi karibuni kutokana na ukweli kwamba bunge letu sasa ni kikaragosi cha serikali, ni asilimia 16 ya VAT kwa mkate, ushuru mpya kwa pikipiki za boda boda zinazoagizwa, asilimia 2.5 ya ushuru wa magari (kutegemea na thamani ya gari), na ushuru mpya wa ikolojia (mazingira).

Wenye nyumba za kupangisha nao hawajasazwa nyuma kwani watahitajika kulipa Ushuru wa Nyumba wa asilimia 1.5.

Inapozingatiwa kuwa Wakenya, hasa walioajiriwa tayari wananing’inia katika hatari ya kukosa mapato, kushindwa kulipa mikopo na kumudu mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, kodi na karo, serikali razini haifai kuanzisha kodi mpya bali kupunguza zile zilizopo.

Hili linafanyika huku wenye ajira wakitarajiwa kuanza kukatwa asilimia 2.75 ya ada ya Bima ya Hospitali (SHIF) kuanzia mwezi wa Julai.

Kinyume na mkakati wa kuzidisha ushuru wa serikali ya Kenya Kwanza, wataalamu wamekuwa wakipendekeza kupunguzwa kwa gharama ya maisha na kubuni nafasi za kazi kama njia pekee ya kumaliza matatizo ya kiuchumi yanayoikumba nchi hii.

Serikali inapopania kuongeza ushuru huku ikitangaza kukatiza au kupunguza ufadhili hasa kwa sekta ya elimu kama vile mpango wa Lishe Shuleni na mkopo wa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya wastani (HELB), kwa upande mwingine imekusudia kuongeza mgao wa idara za serikali zisizokuwa na uhitaji.

Afisi ya Naibu wa Rais, kwa mfano, imetengewa Sh2.6 bilioni kwa matumizi yanayoweza kutajwa kama anasa.

Athari ya ushuru huo ni wazi. Ajira zitaadimika maadamu kampuni nyingi zitafungwa.

Aidha, tutarajie kushuhudia wawekezaji zaidi wakitoroka nchi. Hayo ni baadhi tu ya matokeo mabaya ya ushuru huo.

Baadhi ya kampuni zimetangaza kuwa ziko katika hatari ya kupata hasara.

Ushuru unaoziumiza zaidi nyingi ya kampuni hizo zinazoajiri Wakenya wengi ni Ushuru wa Ada ya Nyumba.

Hapa mwajiriwa hutoa asilimia 1.5 ya mshahara wake nayo kampuni ikijaliza pesa hizo kwa asilimia sawa na hiyo.

Kampuni hizi zitakapowafuta wafanyakazi, mosi serikali ya Kenya Kwanza itapoteza Ushuru wa Mshahara, yaani PAYE, pamoja na makato ya NSSF na hata hiyo ada ya nyumba.

Mwisho hasara kubwa itakuwa kwa serikali kwani watu wengi watakosa kazi ilhali gharama ya maisha itakuwa imeongezeka, hali itakayochangia maovu mengi kufanyika.

Hayo matrilioni ambayo serikali inatarajiwa kukusanya yatapungua kwa sababu biashara zitakuwa zimefungwa nazo kampuni zitakuwa zimefuta wafanyakazi. Serikali itakuwa imetupa jongoo ni mti wake.

Basi Serikali ya Ruto ilihitaji kufanya nini? Kuboresha mazingira ya kibiashara ambayo baadaye yangeajiri Wakenya wengi ambao nao wangeingia katika mduara wa kulipa ushuru.