TAHARIRI: Kila msafiri analo jukumu la kujilinda

TAHARIRI: Kila msafiri analo jukumu la kujilinda

KITENGO CHA UHARIRI

NI rasmi kuanzia leo matatu zitaanza kubeba abiria kama ilivyokuwa zamani.

Wizara ya Uchukuzi ilikubaliana na wamiliki wa matatu kwamba watajidhibiti kwa kubuni mipango ya kukabili corona.

Hatua hii ni habari njema kwa sekta ya matatu ambayo imepata hasara kwa karibu miaka miwili sasa.

Kulipogunduliwa kisa cha kwanza cha maambukizi, serikali kupitia wizara ya Afya ilitangaza kanuni za kuzingatiwa. Kanuni hizo mbali na watu kunawa mikono au kupakwa sanitaiza mikononi, iliagiza abiria wapunguzwe. Matatu za kubeba watu 14 zilianza kubeba wanane.

Kampuni nyingi za mabasi zilijaribu kuunda upya magari yao. Lakini katika kuzingatia kanuni hizo, kampuni za mabasi kama Mombasa Raha na Modern Coast zililazimika kufunga. Hali ni tofauti na ilivyo kwenye uchukuzi wa garimoshi. Abiria kwenye garimoshi kati ya kituo cha Reli cha Nairobi na maeneo ya jiji hujazana hadi wengine wakasimama.

Mambo si tofauti katika vituo vya SGR na ndani ya treni yenyewe. Hata maeneo ya watu kunawa mikono siku hizi hayana sabuni. Hakuna eneo la watu kuchovya sanitaiza. Eneo la kusubiri treni watu huketi bila kuacha nafasi. Wanapoingia ndani hali ni sawa na hiyo.

Kwa hivyo kuwaruhusu abiria kujazana kwenye matatu na mabasi halitakuwa jambo geni.

Kulegezwa kwa kanuni hizi kunafanywa wakati ambapo wimbi la nne la corona limelaza wengi hospitalini. Corona aina ya Delta kutoka India inasemekana kuwa hatari zaidi. Hospitali nyingi nchini zimejaa wagonjwa wanaohitaji kuwekewa mitungi ya hewa ya kupumua.

Hata kudungwa chanjo hakuzuii mtu kupata maradhi hayo. Kusaidia kupunguza tu makali ya ugonjwa wenyewe. Iwapo mtu hajawahi kuishiwa na pumzi, hataelewa umuhimu wa kuepuka maambikizi.

Uhuru wowote huandamana na majukumu. Kuruhusiwa kujazana kwenye magari ya usafiri wa umma kusiwe ni ruhusa ya kupuuza masharti. Corona husambaa kupitia pumzi, mate na majimaji mengine. Kwa hivyo muhimu zaidi kwa abiria ni kuhakikisha wamevaa barakoa wakati wowote. Na wanapokuwa ndani ya magari, wasishike pua, macho au midomo kwa mikono yao.

Kwa njia hii, itakuwa rahisi kuepuka kupatwa na ugonjwa huu ambao kutibiwa ni gharama.

You can share this post!

Kanisa linaloruhusu ndoa za watoto lamulikwa na UN

ONYANGO: Nauli zipunguzwe kufuatia agizo la kujaza abiria...