Makala

TAHARIRI: Kila mtu asome BBI bila shinikizo

October 22nd, 2020 2 min read

Na MHARIRI

BAADA ya kuzinduliwa rasmi kwa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) Jumatano, sasa ni wakati mwafaka kwa viongozi kuwapa Wakenya nafasi kuisoma na kufanya maamuzi huru kuihusu bila shinikizo zozote.

Tangu mchakato wa maandalizi ya ripoti hiyo kuanza, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wamekuwa wakisisitiza lengo lake kuu ni kuiunganisha nchi.

Ni kwa mantiki hiyo ambapo wamekuwa wakiwarai Wakenya kuiunga mkono, wakiahidi itakuwa tiba kwa masuala ambayo yamekuwa yakizua migawanyiko ya kikabila na ushindani usiofaa wa kisiasa.

Hata hivyo, tayari tofauti zimeanza kujitokeza baina ya viongozi kuihusu, baada ya Naibu Rais William Ruto kukosa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wake katika Ikulu Ndogo ya Kisii.

Kimsingi, huu ni mchakato muhimu unaopaswa kutoa nafasi kwa kila Mkenya kueleza hisia zake kuhusu masuala mbalimbali yaliyorejelewa kwenye ripoti hiyo.

Viongozi wanapaswa kuweka kando tofauti zao ili kuhakikisha wanawapa Wakenya mazingira tulivu kuisoma. Halitakuwa jambo mwafaka kwa wanasiasa kuendeleza mikutano ya kuipinga ama kuiunga mkono, kwani hilo litakuwa sawa na kuingilia uhuru wa Wakenya kufanya maamuzi yao.

Wito wetu kwa Rais Kenyatta, Bw Odinga na Dkt Ruto ni kushauriana na washirika wao kisiasa, ili nao pia wajiepushe kuzua taharuki zisizofaa za kisiasa kupitia mikutano hiyo.

Kama nchi inayozingatia demokrasia, wale wanaounga mkono wanapaswa kupewa nafasi yao kujieleza, sawa na wale watakaojitokeza kuipinga.

Sauti zote zitakuwa muhimu, kwani huenda kauli zikajumuisha mapendekezo ambayo yataiboresha hata zaidi. Uwepo wa mazingira tulivu hautatoa nafasi tu kwa wananchi kuisoma na kuielewa, bali pia utazipa nafasi taasisi muhimu kama Bunge la Kitaifa na Seneti kutathmini vipengele ambavyo zitahitajika kuvipitisha.

Katika kuijadili, taasisi hizo pia zinapaswa kuweka maslahi ya Wakenya mbele, badala ya kufanya maamuzi kuihusu kwa kuzingatia misukumo ya kisiasa.

Watakaoiunga mkono wafanye hivyo kwa kuzingatia hoja zilizopo, sawa na wale watakaoipinga. Ni muhimu kwa kila kiongozi kufahamu kwamba huu ni mchakato unaohusu mustakabali wa nchi, wala si mwanasiasa ama kundi la wanasiasa.

Hili ndilo litahakikisha tumeendesha mchakato huo kwa uadilifu kama taifa linaloheshimu maoni na hisia za kila upande.