Makala

TAHARIRI: Kimanzi adhihirishe ufaafu wake Jumapili

September 7th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

MAKALI ya kocha mpya wa Harambee Stars, Francis Kimanzi yanatiwa kwenye mizani Jumapili pale timu ya soka ya Kenya itakabiliana na mahasimu wake wa tangu jadi Uganda Cranes katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Huu ni mchuano wa kwanza kwa kocha huyo aliyechukua mahali pa Mfaransa Sebastien Migne, ambaye alikosa kuvumisha Kenya katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) na mechi za kufuzu kwa kabumbu ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) mwezi jana.

Migne alionekana kushindwa katika harakati ya uteuzi wa kikosi pamoja na kuwapanga wanasoka uwanjani; aghalabu akiwapanga wanasoka wasioelewana vizuri huku wanaofahamiana na wenye tajriba mchezoni wakisahaulika.

Mtihani mkuu wa Kimanzi kesho ni kucheza kete zake kwa uangalifu hasa inapozingatiwa kuwa Uganda ina mchezo mzuri zaidi ukilinganisha na Kenya. Kadhalika, Kenya imekuwa ikisumbuliwa sana na Uganda katika mechi za miaka ya hivi majuzi.

Ushindi katika kandanda ya siku hizi hutokana na maarifa pamoja na uthabiti wa mwili wa wachezaji. Mataifa mengi yaliyong’ara katika fainali za Kombe la Afrika zilizokamilika nchini Misri hapo Julai, yalikuwa na wachezaji walioonekana wenye afya na stamina.

Hivyo basi, ni muhimu kwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuanzia leo Jumamosi kuhakikisha kuwa afya ya wanasoka wa Harambee Stars inatunzwa vizuri.

Hilo linaweza kufaulu tu iwapo wachezaji watalipwa pato zuri mbali na kufuatiliwa kwa karibu kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa mazoezi yao ni ya hadhi ya juu.

Sharti wanasoka hawa pamoja na benchi la ufundi walipwe vizuri na kwa wakati ufaao kama njia moja ya kuwatia motisha.

Wala mechi za kirafiki zisiishie hapo; FKF kwa ushirikiano na serikali yafaa ipange utaratibu wa kuhakikisha kuwa Kenya inapimana nguvu na timu nyingine kubwa mfano wa Nigeria, Ghana, Senegal na hata mabingwa wa Afrika, Algeria.

Kimanzi kwa upande wake sharti awaondoe vijana wetu uoga kama ule ulioshuhudiwa kwenye AFCON ambapo Stars iliegemea mchezo wa kuzuia kila mara ilipokutana na miamba wa Afrika; Algeria na Senegal.

Mwishowe, pasiwepo uteuzi wa kikosi kwa mapendeleo kama ilivyowahi kushuhudiwa mara kadhaa; wanasoka wa Harambee wafaa wateuliwe kutegemea ubora wa mchezo wao.