Makala

TAHARIRI: Kinaya Wakenya kufa mabilioni yakiporwa

March 17th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

Inasikitisha kwamba kwa mara nyingine, Wakenya wameripotiwa kufa njaa huku kashfa za mabilioni ya pesa zikiripotiwa kila uchao.

Na sio kuripotiwa kwa visa vya wizi wa pesa pekee, malumbano yamechacha huku baadhi ya watu wakitetea waporaji wachache wa mali ya umma.

Wanapofanya hivi, mamilioni ya raia, wanaotozwa ushuru mkubwa ili pesa hizo zipatikane wanaendelea kufa kwa njaa. Hii inaonyesha kuwa viongozi tulio nao ni katili.

Katili kwa sababu, hakuna anayeshughulikia kwa dhati masikini wanaowapigia kura. Hakuna kiongozi anayewajibika anayeweza kusubiri watu wake wafe kwa njaa.

Kiongozi anayewajibika huwa anawatembelea watu wake mashinani kila wakati kujua shida zinazowakabili na kutafuta njia za kuzitatua mapema kabla hazijasababisha hasara kubwa. Kiongozi anayewajibika hawezi kusubiri hadi kiangazi kiangamize watu wake.

Kiongozi anayejali hawezi kupinga uchunguzi kuhusu wizi wa mabilioni ya pesa. Inasikitisha kwamba pesa zilizodaiwa kuporwa na watu wachache, miongoni mwao viongozi, zinaweza kulisha Wakenya wanaokabiliwa na baa la njaa kwa zaidi ya miaka kumi.

Zikijumuishwa pamoja, pesa zilizodaiwa kuibwa kupitia kashfa za hivi majuzi zinaweza kununulia Wakenya na mifugo wao chakula cha kutosha.

Naam, zinaweza kuchimba mamilioni ya visima vya kuwapa maji kila siku ya mwaka. Zinaweza kuanzisha miradi ya kuwapa chakula iwapo kungekuwa na nia njema ya kufanya hivyo badala ya miradi hewa inayotumiwa kupora pesa.

Kwa sababu hali ya hewa katika maeneo mengi ya nchi yetu sio ya kutegemewa, serikali inafaa kuwa na mikakati ya kukinga raia wake na mikasa.

Mikakati hiyo ni kama kuhakikisha wakulima wetu wanapatiwa motisha wa kukuza chakula zaidi badala ya kuwatesa kwa kuchelewesha malipo au kununua zao lao kwa bei ya kutupa serikali ikisema haina pesa.

Ajabu ya serikali kukosa pesa za kununulia wakulima mbolea ya bei nafuu lakini za kupora zinapatikana! Ajabu ya kukosa pesa za kukabiliana na janga la njaa ilhali za kuandaa dhifa za kifahari zinapatikana.

Wakenya wanapojitokeza kuwasaidia wenzao wanaokabiliwa na njaa wanafaa na ni haki yao, kushinikiza serikali kuweka mikakati, naam, mikakati ya dhati na kwa nia njema, ya kuimarisha ukuzaji na chakula kwa vitendo badala ya maneno matupu.