TAHARIRI: Kiswahili kimeathiriwa pakubwa na sera baguzi

TAHARIRI: Kiswahili kimeathiriwa pakubwa na sera baguzi

NA MHARIRI

TUNAPOENDELEA na maadhimisho ya ‘Lugha za Kiafrika’ juma hili, tumeangazia masuala ainati kuhusu Kiswahili kama mojawapo ya lugha za Kiafrika.

Masuala mengi yameangaziwa tangu siku ya Jumatatu.

Leo hii tutaangazia kipengele cha sera ya lugha nchini Kenya.

Hali ya sasa ya matumizi ya Kiswahili nchini Kenya imeathiriwa pakubwa na masuala mbalimbali tangu enzi za ukoloni. Athari hizi ni za namna tofauti kutoka nchi moja hadi nyingine katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki.

Tukijikita katika taifa la Kenya, wakoloni walipobisha hodi nchini kwa kuongozwa na kasumba kwamba Kiswahili ilikuwa ni lugha iliyotumiwa katika usambazaji wa dini ya Kiislamu, na maadamu wao walikuwa Wakristo, walipigia debe matumizi ya Kiingereza katika asasi za elimu na kiutawala kisha wakaruhusu matumizi ya lugha za mama katika elimu ya ngazi za chini shuleni.

Hatua hii ilibagua Kiswahili kwa kuisawiri kama lugha isiyostahili japo ndiyo iliyokuwa lugha iliyofahamiwa na watu wa makabila mbalimbali.

Baada ya Kenya kujipatia uhuru, tume nyingi za Elimu zilizoundwa kufanyia uchunguzi masuala mbalimba ya elimu zilitoa mapendekezo ambayo yalikihujumu Kiswahili.

Awali, baadhi ya mapendekezo yalidumisha kasumba za kikoloni kuhusu Kiswahili. Kiingereza kilikwezwa kihadhi na lugha ya Kiswahili ikafanywa somo la hiari katika elimu shuleni.

Ni katika mwaka wa 1984 wakati wa kuzinduliwa kwa mfumo wa elimu wa 8.4.4 ambapo hatua muhimu sana katika ukuzaji wa Kiswahili ilipigwa. Tume iliyopendekeza mfumo huu iliamua kwamba Kiswahili mbali na kwamba ni lugha ya taifa, kifanywe somo la lazima kuanzia shule za msingi hadi za sekondari. Hii ilikuwa hatua kubwa sana tena ya kizalendo.

Licha ya hatua hii ya 8.4.4 iliyopigwa jeki na Katiba mpya ya mwaka wa 2010 ya kukifanya Kiswahili lugha rasmi ya kwanza nchini, Kiswahili bado hakijapewa hadhi inayostahili. Masalia ya kasumba za kikoloni na sera baguzi zinazokitazama Kiswahili kama lugha ya watu ambao hawakusoma zinaendelea kukandamiza Kiswahili.

Bado zipo baadhi ya sera za lugha katika baadhi ya shule humu nchini ambazo zinatoa adhabu kali kwa mwanafunzi yeyote anayepatikana akizungumza Kiswahili. Baadhi ya shule zinazojiita za kimataifa hazifundishi kabisa kabisa Kiswahili.

Ni kwa mintarafu hii ambapo suluhisho kwa nyingi za changamoto ambazo Kiswahili kinapitia zinafaa kukitwa katika sera za Kitaifa ili kuitumikisha barabara lugha hii ashirafu.

You can share this post!

Kalonzo sasa apanda bei

Hofu mapinduzi yakizuka upya Afrika Magharibi

T L