Makala

TAHARIRI: Klabu za NSL, KPL zianze kujidhamini

November 9th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

MWANZONI mwa wiki hii, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), liliamuru kuahirishwa kwa mechi zote za kikosi cha Northern Wanderers FC kilichokuwa kikiwania ubingwa wa Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza (NSL).

Meneja wa mashindano wa FKF alimtaka Frank Ogola ambaye ni Mwenyekiti wa NSL kuwaondoa Wanderers FC katika orodha ya wawaniaji wa ubingwa wa taji hilo na nafasi yao kujazwa na Eldoret Youth.

Hadi kuwasilishwa kwa ombi la kuondolewa kwa Wanderers ligini baada ya ubovu wa hali yao ya kifedha kuwaweka katika ugumu wa kujiendesha, kikosi hicho hakikuwa kimesajili ushindi wowote katika kampeni za NSL msimu huu.

Uchechefu wa fedha ni suala ambalo linazidi pia kutatiza vikosi vingi vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Mathare United ambao ni mabingwa wa 2008, Chemelil Sugar, SoNy Sugar ambao ni mabingwa wa 2006, Kakamega Homeboyz, Kisumu All Stars na Kariobangi Sharks ni miongoni mwa klabu ambazo zimekuwa zikitaka wasimamizi wa KPL kusitisha kivumbi hicho kuanzia hadi changamoto za kifedha zinazowakabili wawaniaji wa ubingwa wa kipute hicho zitatuliwe.

KPL kwa sasa inapitia panda-shuka tele tangu SportPesa ambao walikuwa wadhamini wa Ligi Kuu wasitishe shughuli zao zote katika soko la humu nchini. Maombi ya klabu hizi kutaka kipute cha KPL kisitishwe ni zao la hali ngumu ya kifedha inayochangia uzito wa kujiendesha kwa vikosi husika vinavyotatizika kugharimia mishahara ya wachezaji.

Wachezaji wa klabu mbalimbali hawajalipwa kwa miezi kadhaa sasa, na madhara makubwa yalishuhudiwa hivi maajuzi baada ya klabu za Chemelil na SoNy kushindwa kucheza mechi zao muhimu dhidi ya Bandari FC na AFC Leopards mtawalia.

Hali imekuwa mbaya na kusababisha viongozi wa KPL kuamua kuwa klabu sasa zigharamie malipo ya waamuzi wanaochezesha mechi mbalimbali. Hii ni hatari sana kwa maendeleo ya soka nchini. Ukweli ni kwamba, uamuzi huu wa wasimamizi wa ligi unamaanisha kuwa kuna waamuzi ambao tangu kuanza kwa msimu huu, hawajalipwa mshahara wao.

Kwa kweli, tumekuwa tukishuhudia changamoto za kifedha katika ligi kuu katika miaka iliyopita, lakini, inavyoonekana kwa sasa, hali imekuwa mbaya zaidi na suluhisho la kudumu linastahili kupatikana.

Kwanza, kinachotokea kinaonyesha kuwa, klabu zetu hazina msingi mzuri wa kifedha. Tumesalia wategemezi kwa wafadhili au watu binafsi ili kufanikisha shughuli za mchezo wa soka. Tulianza kuteseka miaka kadhaa iliyopita, baada ya kujiondoa kwa SuperSport ya Afrika Kusini.

Hawa ni wafadhili waliokuwa wanatoa fedha zao kusaidia kuendesha ligi lakini pia, walikuwa wanaonyesha moja kwa moja mechi kadhaa za ligi.

Hata hiyo, kitendo cha viongozi wa soka nchini kutangaza kuongeza idadi ya timu zinazoshiriki, wakati huo kutoka 16, ziliwafukuza wafadhili hao na tukasalia bila chochote, na hivi punde ni suitafahamu kati ya serikali na kampuni ya SportPesa.

Hali kama hii inapotokea, wanaoumia ni wachezaji. Soka siku hizi ni ajira. Wachezaji wengi wanategemea kucheza soka ili walipwe mshahara ili kuzisaidia familia zao.

Lakini, hali inapokuwa hivi, inabidi watafute kitu kingine cha kufanya na hivyo, soka inakuwa shughuli ya pili, na tunapoanza kushuhudia hili, ina maana kuwa kiwango cha soka kitaanza kushuka. Kutatua tatizo hili, klabu zetu zianze kufikiria miradi ambayo inaweza kusaidia kuwa na msingi mzuri wa fedha ili kuepuka hali kama hii.