TAHARIRI: Kongole kwa mashujaa wetu waliofana Brazil

TAHARIRI: Kongole kwa mashujaa wetu waliofana Brazil

NA MHARIRI

TUNAWAPA pongezi tele mabingwa wa Olimpiki ya Viziwi mwaka huu ambao walirejea nyumbani mnamo Alhamisi kutoka jijini Caxias do Sul, Brazil.

Ni fahari tele baada ya Wakenya hawa mashujaa kuzoa medali fufufu katika mashindano hayo, ikiwemo medali ya kwanza kabisa ya Kenya katika mchezo wa gofu.

Isaac Makokha amejiweka kwenye mabuku ya historia ya Kenya kwa kuletea taifa shaba ya gofu – Kenya haikuwa imepata medali yoyote katika mashindano ya kimataifa ya gofu.

Aidha, pongezi za dhati tunazitoa kwa mabingwa hawa waliojikakamua zaidi ya mno kuzoa medali hizo, na wale pia ambao hawakufanikiwa kuzoa chochote, ikizingatiwa kuwa kikosi hicho kilikumbana na changamoto si haba katika maandalizi yake.

Itakuwa vyema kuwataja wanaume na wanawake hawa wa taifa kwanza kwani walishinda upungufu wa kimaumbile sio tu kushiriki mashindano lakini pia kuibuka bora barani Afrika na nambari 10 duniani.

Waliojishindia dhahabu ni: Lucas Wandia katika 3,000m kuruka viunzi na maji; Symon Kibai 5,000m na 10,000m; Ian Wambui 1,500m; na Elikana Kiprop Rono 800m.

Fedha ziliwaendea Peter Toroitich 10,000m; Searah Wangari 10,000m; Sharon Bitok 1,500m; Ian Wambui 5,000m; Sharon Bitok 800m; George Waweru, Linet Fwamba, Beryl Wamira na Isaac Atima mbio za kupokezana vijiti kwa timu mseto; na Beryl Wamira, Linet Fwamba, Pamela Atieno na Sharon Bitok mbio za kupokezana vijiti za 4x400m.

Mashujaa wetu waliojinyakulia shaba ni pamoja na David Kipkogei 10,000m; Grancy Kendagor 1,000m; Kelvin Kipkogei kurusha mkuki; Linet Fwamba 400m; Isaac Makokha gofu; Peter Omari Kokobi 3,000m kuruka viunzi na maji; Ann Njoki Wangeci 3,000m kuruka viunzi na maji; Berly Wamira 200m; Relay – Beryl Wamira, Rael Wamira, Anzazi Chaka na Linet Fwamba mbio za kupokezana vijiti za 4x100m; Rebecca Matiko 800m; Grancy Kendagor 5,000m; na Simon Menza Gona, Charles Muthama Mwema, George Waweru Muthee na Isaac Atima Tongi mbio za kupokezana vijiti za 4x400m.

Kikosi hicho kilifana ikilinganishwa na makala ya 2017 mjini Samsun, Uturuki, ambapo taifa lilizoa medali 16; dhahabu tano, fedha tano na shaba sita.

Tunatumai serikali itasikia ombi lao iwape vifaa maalum wanavyohitaji katika mazoezi na pia kukuza michezo yao mashinani, ihakikishe wanaanza maandalizi miezi miwili kabla mashindano wala sio wiki tatu kama ilivyokuwa kwa kikosi cha sasa; na kuwapa ajira katika vikosi vya usalama na taasisi za serikali wanazowakilisha, kama ambavyo inafanyika kwa wanamichezo wenzao wasio na ulemavu.

You can share this post!

Aliyefutwa kwa kuugua afidiwa laki 2

Huenda IEBC ikamwidhinisha Kalonzo kuwania urais kivyake

T L